News
Hofu ya Ongezeko la HIV
Shirika la umoja wa mataifa la kupambana na virusi vya UKIMWI, UNAIDS, limesema huenda kukawa na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi milioni 6 na vifo milioni 4 vinavyohusiana na ukimwi kufikia mwaka 2029.
Hii ni kutokana na kupunguzwa kwa fedha za misaada ya kiafya kutoka Shirika la Marekani, USAIDS.
Kulingana na takwimu, taifa la Afrika kusini ndio taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi ulimwenguni lakini pia nchi inayoongoza katika utafiti wa virusi vya ukimwi ulimwenguni.
Miongoni mwa mataifa mengine, Afrika kusini pia imekuwa nchi ambayo pia ilikuwa ni mpokeaji mkubwa wa fedha za UKIMWI kutoka Marekani hadi Machi mwaka huu, wakati utawala wa Rais Trump ulipotangaza kufungwa kwa Shirika la USAID.
Mwezi uliopita vyuo vikuu vya juu vya Afrika Kusini viliomba serikali madola ya mamilioni ili kuendelea na utafiti huu ambao baadhi umesitishwa kwa sababu ya kupunguzwa kwa fedha na Marekani.
Pesa hii ilisaidia nchi hiyo kupunguza kiwango chake cha maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi kwa zaidi ya asilimia 60 tangu kilele chake mnamo 2000.
Siku ya Jumatano tarehe 9 Julai 2025, serikali ya Afrika Kusini na wafadhili wa kimataifa waliahidi karibu dola milioni 54 ili kukabili palipo na mapungufu.
Mwaka jana Marekani ilitumia mara nane ya kiwango hicho kwa ufadhili wa Virusi Vya Ukimwi Afrika Kusini kiwango hiki hakitatosha kutimiza hitaji lililopo.
Taarifa ya Hamis Kombe
News
Rais Ruto atia saini kuwa sheria mswada wa hazina ya uwekezaji wa mali
Rais William Ruto ametia saini kuwa sheria mswada wa hazina ya kitaifa ya uwekezaji wa mali (Sovereign Wealth Fund), hatua inayotajwa kuwa muhimu katika juhudi za Kenya za kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, kulinda utajiri wa taifa na kuchochea ukuaji wa uchumi wa muda mrefu.
Utiaji huo wa saini ulifanyika katika Ikulu ya Nairobi na unaweka msingi wa kisheria wa kuanzishwa na kusimamiwa kwa mfuko wa taifa wa uwekezaji wa mali na kwamba unatarajiwa kuiwezesha nchi kuhifadhi rasilimali za umma zinazobaki baada ya matumizi ya kawaida, kufadhili uwekezaji wa kimkakati na kuimarisha uwezo wa uchumi kukabiliana na misukosuko ya kifedha siku zijazo.
Sheria hiyo mpya inaleta mfumo rasmi wa usimamizi wa utajiri wa taifa kwa kutenga akiba kwa ajili ya vizazi vijavyo, kuimarisha uthabiti wa uchumi na kufadhili uwekezaji katika miundombinu ya kimkakati ili kuongeza uimara wa kifedha nchini pamoja na kuhimiza matumizi yenye uwajibikaji ya rasilimali za umma.
Mfuko huo utatumika kuwekeza mapato ya ziada yanayotokana na rasilimali za asili na mali nyingine za umma, kwa lengo la kuhakikisha manufaa yake yanawanufaisha wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.
Aidha, mfuko huo unakusudia kupunguza athari za changamoto za kiuchumi kwa kutoa kinga ya kifedha wakati wa misukosuko ya uchumi.
Sheria hiyo ni sehemu ya ajenda pana ya serikali ya mageuzi ya uchumi inayolenga kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, kuongeza uwazi na kuendeleza maendeleo endelevu.
Pia, sheria hiyo imeweka mfumo wa uongozi na usimamizi wa mfuko huo, ukiwemo utaratibu wa kuhakikisha uwajibikaji, uwazi na usimamizi madhubuti katika uwekezaji na matumizi ya rasilimali za umma.
Maafisa wa serikali wameeleza kuwa Mfuko wa Taifa wa Uwekezaji wa Mali utakuwa na mchango mkubwa katika kufadhili miradi ya maendeleo yenye kipaumbele nchini huku ukihifadhi utajiri wa taifa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Kupitishwa kwa sheria hiyo kunaiweka Kenya miongoni mwa mataifa yanayoongezeka duniani ambayo yameanzisha mifuko ya taifa ya uwekezaji wa mali kwa lengo la kulinda mali za taifa, kuimarisha uthabiti wa uchumi na kufadhili malengo ya maendeleo ya muda mrefu.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
IEBC yakosolewa dhidi ya masharti mapya kwa wanasiasa
Kiongozi wa vijana katika Chama cha Wiper kaunti ya Kwale Nyawa Masai ameikosoa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kutokana na masharti mapya iliyotoa dhidi ya wanasaisa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Nyawa ameitaka Tume hiyo kuzingatia kanuni zake na taratibu za kuandaa uchaguzi na wala sio kila uchao kutoa masharti ambayo yanakinzana na majukumu ya Tume, akisema kuna taasisi zengine za umma zinafaa kuwajibika.
Akizungumza katika mkutano wa kisiasa katika eneo la Mwereni gatuzi dogo la Lungalunga kaunti ya Kwale, Nyawa aliesisitiza haja ya wanasiasa kupewa nafasi ya kuzungumza na wananchi sawa na kueleza sera zao bila ya vizuizi.
Kiongozi huyo wa vijana ambaye alitangaza nia yake ya kuwania kiti cha uwakilishi wadi ya Mwereni wakati wa uchaguzi ujao, amesema taifa la Kenya linazingatia demokrasia na kwamba kila taasisi inafaa kutekeleza majukumu yake.
“Katika uwaja wa siasa IEBC inakuzi moja tu kama msimamizi na kama msimamizi anaanza kutengeza sheria hapo ndipo anakosea, hii Kneya ni nchi ya demokrasia kwa hivyo IEBC isilete sheria nyingi na kufuatilia wanasiasa kuhusu pesa watatumia kwa kampeni, hiyo sio jukumu lake kuna taasisi inaitwa EACC”, alisema Nyawa.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

