News
Imarika Sacco yazindua kampeni ya Ekeza na ushinde–Imarika gari promotion
Wateja na wanachama wa shirika la uekezaji na mikopo la Imarika Sacco walijumuika na maafisa na shirika hilo katika maeneo mbali mbali kaunti ya Kilifi kwenye kampeni ya kuwahamasisha kuhusu kuekeza na kujishindia zawadi chungu nzima.
Vivile vile wateja hao pamoja na mashabiki wa kituo hiki cha Coco fm walipata fursa ya kukutana na watangazaji moja kwa moja katika msafara ulioanza eneo la Gongoni, kuelekea Malindi, Gede, Watamu, Mastangoni na kutamatika eneo la Mkoroshoni Mjini Kilifi.
Kulingana na afisa mthibiti wa akiba Agricola Ngeti kutoka shirika la Imarika Sacco, kampeni hiyo iliyopewa jina Ekeza na ushinde–Imarika gari promotion iling’oa nanga kuanzia tarehe saba mwezi wa Julai, 2025 hadi tarehe 30, Novemba 2025.
Ngeti alisihi wanachama na wale ambao hawajajisajili na shirika hilo kufanya hivyo na kuekeza zaidi, ili kupata fursa ya kujishindia zawadi.
“Kwa mwanachama yeyote ambaye ambaye atataka kwa hili shindano anafaa aekeze kiwango cha chini cha shilingi 1,000, lakini inatakikana ile pesa ambayo unaekezxa kila mwezi iwe zaidi ya chenye mwanachama ataekeza ndio aingine kwenye shindano, zaidi anavyoendelea kuekeza ndio anakaribia kuwa mshindi, kwa wale wanachama ambao watakuwa watatu kwa washindi wa wiki watashinda 5,000 wale washindi wa mwezi tutachukua 2,000 tutapeleka kwa share capital, halafu mshindi wa kwanza atapewa gari, wapili atapewa tuktuk na watatu atapewa pikipiki”, alisema Bi Ngeti

Baadhi ya waliojitokeza kwenye msafara wa Imarika Sacco na Coco Fm Gongoni.
Ngeti aliongeza kuwa mesema lengo kuu la kampeni hiyo ni kusaidia wanachama kuekeza zaidi na kufaidika na mikapo.
“Tunasaidia wanachama wetu waekeze zaidi wapate mikopo na sisi kama Sacco tuwe na pesa nyingi ambazo tunaweza kukopesha wanachama wetu”, aliongeza Ngeti

Umati uliojitokeza kwenye kampeni ya Ekeza na ushinde–Imarika gari promotion eneo la mkoroshoni Kilifi.
Baadhi ya wateja waliojisajili na shirika hilo akiwepo Samuel Kifalu wameeleza matumaini na kunufaika na huduma za uekezaji katika shirika hilo la Imarika Sacco.
“Nimefungua akaunti nataka kujiekezea ili kuanza biashara, nazieka kwenye akaunti ikifika kiwango cha kupewa mkopo nianze biashara ya kujiendeleza, Imarika Sacco iko sawa, kwa mwezi natarajia kuweka kama shilingi 5,000, nataka kushinda hata kama nigari ama tuktuk au pikipiki”, Alisema Kifalu.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Polisi wanachunguza tukio la wizi dhidi ya raia wa kigeni
Maafisa wa Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza tukio la wizi dhidi ya mtalii wa kigeni lililotokea katika eneo la Nyali
Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, mtalii huyo mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni raia wa Marekani, anadai kulaghaiwa na kisha kushambuliwa na kundi la wanaume aliyokutana nao muda mfupi kabla ya tukio.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba mnamo mwezi Aprili 9 mwaka huu, raia huyo wa kigeni akiwa katika mkahawa mmoja eneo la Nyali jijini Mombasa, alikutana na mwanaume aliyejitambulisha kama Alex, ambaye alimshawishi kuelekea katika nyumba ya Airbnb iliyoko karibu na mkahawa huo.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kwamba alipofika katika chumba hicho, alikumbana na wanaume wengine watano waliokuwa wakimsubiri ambapo mlango ulifungwa na kisha akashambuliwa na kulazimishwa kutoa pesa na vitu vya thamani.
Wahalifu hao walitoroka na mali mbalimbali ikiwemo simu ya rununu, kompyuta mpakato (laptop), fedha taslimu pamoja na fedha za kigeni na pia walifanikiwa kutoa pesa kutoka kwenye kadi zake za benki kwa njia ya udanganyifu.
Maafisa wa polisi kutoka Bamburi kwa kushirikiana na maafisa wa upelelezi wa DCI Nyali walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, ingawa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa wala mali iliyopatikana.
Kesi hiyo imewekwa chini ya uchunguzi zaidi huku juhudi zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Polisi eneo la Likoni-Mombasa inachunguza kifo cha mwanamke
Idara ya usalama eneo la Likoni kaunti ya Mombasa imesema inachunguza kifo cha mwanamke mmoja aliyefariki katika mtaa wa senti kumi.
Mkuu wa polisi wa Likoni Joseph Mutungi alisema mwanamke huyo anadaiwa kupoteza maisha wakati wakiwa nyumbani kwa mwanamme anayesemekana kuwa mchumba wake.
Taarifa za awali ziliarifu kuwa marehemu alikuwa mgonjwa na anadaiwa alifika hospitalini kusaka matibabu japo hakupata huduma na kurejea nyumbani bila kutibiwa.
Inasemekana baadaye mchumba wake alioondoka kwenda kazini na kumwacha chini ya uangalizi wa mwanamke mwengine katika ploti hiyo.
Hali yake inadaiwa kuzorota na hatimaye kuaga dunia.
Maafisa wa usalama walisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Coast general kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

