News
Kadinali Farrell: Papa Francis Atazikwa Jumamosi Aprili 26
Uongozi wa Kanisa Katoliki mjini Vatican umetangaza kwamba Papa Francis atazikwa siku ya Jumamosi Aprili 26 katika Kanisa kuu la mtakatifu Bikiri Maria mkuu kuanzia mwendo wa saa nne asubuhi kwa kuambatana na Ibada ya Misa.
Kulingana na Kadinali Kevin Farrell, Camerlengo wa baraza la kitume la Kanisa Katoliki, uamuzi huo umeafikiwa kufuatia mkutano wa makadinali wote waliowasili Vatican kwa mipingo na maadilinzi ya mazishi kabla ya waumini wa Kanisa Katoliki kuruhusiwa kuutazama mwili wa Papa.
Kadinali Farrell amesema kwa kuzingatia kanuni na desturi za Kanisa Katoliki baada ya Papa kuaga dunia, Kanisa limefunga makaazi ya Papa kwa kitambaa chekundu kuashiria kwamba Papa amefariki na mwili wake umewekwa ndani ya jeneza katika Kanisa la Casa Santa Marta mjini Vatican huku maombi maalum yakiendelea.
Kulingana na desturi za Kanisa Katoliki baada ya mazishi makadinali watakusanyika pamoja katika chumba maalamu yaani Conclave ili kuanza mchakato wa kumchagua Papa mpya katika kipindi cha siku 15 hadi 20 na mchakato huo umepangwa kuanza rasmi mwezi Mei tarehe 5.
Pete ya Papa Francis, pia huvunjwa na kuharibiwa ishara ya ukomo wa maisha yake ya Papa.
Itakumbukwa kwamba Papa Francis aliaga dunia mnamo siku ya Jumatatu Aprili 21 mwendo wa saa moja na nusu asubuhi baada ya kuugua dunia akiwa na umri wa miaka 88.
News
Polisi wanachunguza tukio la wizi dhidi ya raia wa kigeni
Maafisa wa Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza tukio la wizi dhidi ya mtalii wa kigeni lililotokea katika eneo la Nyali
Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, mtalii huyo mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni raia wa Marekani, anadai kulaghaiwa na kisha kushambuliwa na kundi la wanaume aliyokutana nao muda mfupi kabla ya tukio.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba mnamo mwezi Aprili 9 mwaka huu, raia huyo wa kigeni akiwa katika mkahawa mmoja eneo la Nyali jijini Mombasa, alikutana na mwanaume aliyejitambulisha kama Alex, ambaye alimshawishi kuelekea katika nyumba ya Airbnb iliyoko karibu na mkahawa huo.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kwamba alipofika katika chumba hicho, alikumbana na wanaume wengine watano waliokuwa wakimsubiri ambapo mlango ulifungwa na kisha akashambuliwa na kulazimishwa kutoa pesa na vitu vya thamani.
Wahalifu hao walitoroka na mali mbalimbali ikiwemo simu ya rununu, kompyuta mpakato (laptop), fedha taslimu pamoja na fedha za kigeni na pia walifanikiwa kutoa pesa kutoka kwenye kadi zake za benki kwa njia ya udanganyifu.
Maafisa wa polisi kutoka Bamburi kwa kushirikiana na maafisa wa upelelezi wa DCI Nyali walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, ingawa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa wala mali iliyopatikana.
Kesi hiyo imewekwa chini ya uchunguzi zaidi huku juhudi zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Polisi eneo la Likoni-Mombasa inachunguza kifo cha mwanamke
Idara ya usalama eneo la Likoni kaunti ya Mombasa imesema inachunguza kifo cha mwanamke mmoja aliyefariki katika mtaa wa senti kumi.
Mkuu wa polisi wa Likoni Joseph Mutungi alisema mwanamke huyo anadaiwa kupoteza maisha wakati wakiwa nyumbani kwa mwanamme anayesemekana kuwa mchumba wake.
Taarifa za awali ziliarifu kuwa marehemu alikuwa mgonjwa na anadaiwa alifika hospitalini kusaka matibabu japo hakupata huduma na kurejea nyumbani bila kutibiwa.
Inasemekana baadaye mchumba wake alioondoka kwenda kazini na kumwacha chini ya uangalizi wa mwanamke mwengine katika ploti hiyo.
Hali yake inadaiwa kuzorota na hatimaye kuaga dunia.
Maafisa wa usalama walisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Coast general kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

