News
Kaunti ya Lamu yakabiliwa na changamoto ya nguvu za umeme
Kaunti ya Lamu inaendelea kushuhudia changamoto ya nguvu za umeme ambayo inaendelea kuathiri utoaji wa huduma katika idara mbali mbali katika kaunti hiyo.
Gavana wa kaunti hiyo Issa Timamy alisema kaunti hiyo imelazimika kutumia mitambo ya kunasa miale ya jua maarufu sola ili kutoa huduma mbali mbali kwa wakaazi wa kaunti hiyo.
Kulingana na gavana Timamy hali hiyo imechangiwa na gharama za juu za umeme sawa na kupotea kwa nguvu za umeme mara kwa mara.
Timamy pia alisema visima vikuu vya kusambaza maji katika chemichemi ya maji ya milima ya bahari eneo la Shela vinatumia umeme wa sola kuvuta maji ili yafike majumbani.
Gavana huyo alidokeza kuwa mashine ya kubadilisha maji ya bahari kuwa maji ya kunywa eneo la Mkokoni pia hutumia umeme wa sola na pia taa za barabarani maeneo yote ya Lamu.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Rais Ruto atia saini kuwa sheria mswada wa hazina ya uwekezaji wa mali
Rais William Ruto ametia saini kuwa sheria mswada wa hazina ya kitaifa ya uwekezaji wa mali (Sovereign Wealth Fund), hatua inayotajwa kuwa muhimu katika juhudi za Kenya za kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, kulinda utajiri wa taifa na kuchochea ukuaji wa uchumi wa muda mrefu.
Utiaji huo wa saini ulifanyika katika Ikulu ya Nairobi na unaweka msingi wa kisheria wa kuanzishwa na kusimamiwa kwa mfuko wa taifa wa uwekezaji wa mali na kwamba unatarajiwa kuiwezesha nchi kuhifadhi rasilimali za umma zinazobaki baada ya matumizi ya kawaida, kufadhili uwekezaji wa kimkakati na kuimarisha uwezo wa uchumi kukabiliana na misukosuko ya kifedha siku zijazo.
Sheria hiyo mpya inaleta mfumo rasmi wa usimamizi wa utajiri wa taifa kwa kutenga akiba kwa ajili ya vizazi vijavyo, kuimarisha uthabiti wa uchumi na kufadhili uwekezaji katika miundombinu ya kimkakati ili kuongeza uimara wa kifedha nchini pamoja na kuhimiza matumizi yenye uwajibikaji ya rasilimali za umma.
Mfuko huo utatumika kuwekeza mapato ya ziada yanayotokana na rasilimali za asili na mali nyingine za umma, kwa lengo la kuhakikisha manufaa yake yanawanufaisha wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.
Aidha, mfuko huo unakusudia kupunguza athari za changamoto za kiuchumi kwa kutoa kinga ya kifedha wakati wa misukosuko ya uchumi.
Sheria hiyo ni sehemu ya ajenda pana ya serikali ya mageuzi ya uchumi inayolenga kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, kuongeza uwazi na kuendeleza maendeleo endelevu.
Pia, sheria hiyo imeweka mfumo wa uongozi na usimamizi wa mfuko huo, ukiwemo utaratibu wa kuhakikisha uwajibikaji, uwazi na usimamizi madhubuti katika uwekezaji na matumizi ya rasilimali za umma.
Maafisa wa serikali wameeleza kuwa Mfuko wa Taifa wa Uwekezaji wa Mali utakuwa na mchango mkubwa katika kufadhili miradi ya maendeleo yenye kipaumbele nchini huku ukihifadhi utajiri wa taifa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Kupitishwa kwa sheria hiyo kunaiweka Kenya miongoni mwa mataifa yanayoongezeka duniani ambayo yameanzisha mifuko ya taifa ya uwekezaji wa mali kwa lengo la kulinda mali za taifa, kuimarisha uthabiti wa uchumi na kufadhili malengo ya maendeleo ya muda mrefu.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
IEBC yakosolewa dhidi ya masharti mapya kwa wanasiasa
Kiongozi wa vijana katika Chama cha Wiper kaunti ya Kwale Nyawa Masai ameikosoa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kutokana na masharti mapya iliyotoa dhidi ya wanasaisa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Nyawa ameitaka Tume hiyo kuzingatia kanuni zake na taratibu za kuandaa uchaguzi na wala sio kila uchao kutoa masharti ambayo yanakinzana na majukumu ya Tume, akisema kuna taasisi zengine za umma zinafaa kuwajibika.
Akizungumza katika mkutano wa kisiasa katika eneo la Mwereni gatuzi dogo la Lungalunga kaunti ya Kwale, Nyawa aliesisitiza haja ya wanasiasa kupewa nafasi ya kuzungumza na wananchi sawa na kueleza sera zao bila ya vizuizi.
Kiongozi huyo wa vijana ambaye alitangaza nia yake ya kuwania kiti cha uwakilishi wadi ya Mwereni wakati wa uchaguzi ujao, amesema taifa la Kenya linazingatia demokrasia na kwamba kila taasisi inafaa kutekeleza majukumu yake.
“Katika uwaja wa siasa IEBC inakuzi moja tu kama msimamizi na kama msimamizi anaanza kutengeza sheria hapo ndipo anakosea, hii Kneya ni nchi ya demokrasia kwa hivyo IEBC isilete sheria nyingi na kufuatilia wanasiasa kuhusu pesa watatumia kwa kampeni, hiyo sio jukumu lake kuna taasisi inaitwa EACC”, alisema Nyawa.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

