News
Kenya Yatoa ufadhili wa Asilimia 20 kwa WHO
Kenya imejitolea kuongeza ufadhili wake kwa Shirika la Afya duniani WHO kwa asilimia 20 katika kipindi cha miaka 4 ijayo.
Waziri wa Afya nchini Aden Duale ameyasema hayo wakati wa Kongamano la 78 la Afya duniani linaloendelea mjini Geneva nchini Uswizi, ambapo amesisitiza haja ya serikali ya Kenya kujitolea katika kuboresha sekta ya afya ulimwenguni.
Waziri Duale amesisitiza umuhimu wa ufadhili endelevu kwa Shirika la Afya duniani WHO, akisema licha ya bajeti kurekebishwa na kuweka ufadhili huo mdogo pia utasaidia sekta ya afya.
Waziri Duale ameangazia dhamira ya serikali ya Kenya ya kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma za afya kwa wote UHC, kuimarishwa kwa ufadhili wa afya na kuendeleza miundombinu ya afya ya kidijitali ili kuendesha sera inayotumia data.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amepongeza kujitolea kwa mataifa wanachama katika kufadhili WHO, akisema ahadi zilizotolewa na mataifa hayo zitachangia kuimarika kwa sekta ya afya duniani.
News
Polisi wanachunguza tukio la wizi dhidi ya raia wa kigeni
Maafisa wa Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza tukio la wizi dhidi ya mtalii wa kigeni lililotokea katika eneo la Nyali
Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, mtalii huyo mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni raia wa Marekani, anadai kulaghaiwa na kisha kushambuliwa na kundi la wanaume aliyokutana nao muda mfupi kabla ya tukio.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba mnamo mwezi Aprili 9 mwaka huu, raia huyo wa kigeni akiwa katika mkahawa mmoja eneo la Nyali jijini Mombasa, alikutana na mwanaume aliyejitambulisha kama Alex, ambaye alimshawishi kuelekea katika nyumba ya Airbnb iliyoko karibu na mkahawa huo.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kwamba alipofika katika chumba hicho, alikumbana na wanaume wengine watano waliokuwa wakimsubiri ambapo mlango ulifungwa na kisha akashambuliwa na kulazimishwa kutoa pesa na vitu vya thamani.
Wahalifu hao walitoroka na mali mbalimbali ikiwemo simu ya rununu, kompyuta mpakato (laptop), fedha taslimu pamoja na fedha za kigeni na pia walifanikiwa kutoa pesa kutoka kwenye kadi zake za benki kwa njia ya udanganyifu.
Maafisa wa polisi kutoka Bamburi kwa kushirikiana na maafisa wa upelelezi wa DCI Nyali walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, ingawa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa wala mali iliyopatikana.
Kesi hiyo imewekwa chini ya uchunguzi zaidi huku juhudi zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Polisi eneo la Likoni-Mombasa inachunguza kifo cha mwanamke
Idara ya usalama eneo la Likoni kaunti ya Mombasa imesema inachunguza kifo cha mwanamke mmoja aliyefariki katika mtaa wa senti kumi.
Mkuu wa polisi wa Likoni Joseph Mutungi alisema mwanamke huyo anadaiwa kupoteza maisha wakati wakiwa nyumbani kwa mwanamme anayesemekana kuwa mchumba wake.
Taarifa za awali ziliarifu kuwa marehemu alikuwa mgonjwa na anadaiwa alifika hospitalini kusaka matibabu japo hakupata huduma na kurejea nyumbani bila kutibiwa.
Inasemekana baadaye mchumba wake alioondoka kwenda kazini na kumwacha chini ya uangalizi wa mwanamke mwengine katika ploti hiyo.
Hali yake inadaiwa kuzorota na hatimaye kuaga dunia.
Maafisa wa usalama walisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Coast general kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

