Business
Maonyesho ya Kilimo Mombasa 2025 kuangazia uhifadhi wa mazingira
Washirika kutoka mataifa saba duniani wanatarajiwa kushiriki katika maonyesho ya kimataifa ya kilimo ya mwaka 2025 yanayofanyika eneo la Mkomani kaunti ya Mombasa.
Mwenyekiti wa maonyesho hayo Henry Nyaga, alidokeza kuwa maonyesho hayo yamevutia washirika kutoka mataifa ya afrika mashariki, vile vile mataifa ya India, China, Botswana, Zambia na DR.Congo.
Akizungumza na Coco Fm katika uwanja wa maonyesho hayo, Nyaga alisema maonyesho ya mwaka huu wa 2025 yanaangazia kilimo biashara akisistiza umuhimu wa vijana kushiriki katika hafla hiyo iliyoambatanishwa na matumizi ya teknolojia na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuhifadhi mzaingira.
“Kuna wale kutoka mataifa saba ambao tayari wameonyesha watakuwa nasi, tayari amewasili yule ambaye anatoka nchi ya Botswana, tunazingatia mambo haya ya tabia nchi ambayo yamefanya ulimwengu umekuwa tofauti sasa, kwa hivyo tunatarajia washiriki wote watatuonyesha jinsi gani tunaweza kukabiliana na hali hii ya mabadiliko ya tabia nchi, na ningependa haswa vijana muweze kufika hapa katika maonyesho kwa sababu kuna mengi ya kiteknolojia ambayo yanaweza kuwasaidia”,alisema Nyaga.
Kwa upande wake mwenyekiti wa maonyesho ya kilimo nchini Edith Onzare pamoja na mwanachama wa baraza la maonyesho ya Kilimo Mombasa- Anisa Abdhalla waliwasihi wananchi kutumia fursa hiyo kujifunza mengi kuhusu kilimo endelevu na namna ya kujiendeleza kuhusu ufugaji wa kisasa.
“Njooni kwa wingi tutajifunze mengi ya kilimo, kuna mifugo ya aina mbali mbali kuna kilimo na teknolojia hasa kwa vijana wetu, magen z kuna kazi nyingi ambazo ukija hapa kwenye maonyesho utajifunza mambo mengi ya kiteknolojia na taaluma mbali mbali ambazo utaweza kupata usaidizi”,walisema viongozi hao.
Baadhi ya washirika katika maonyesho hayo walishinikiza wakenya kukumbatia kilimo cha kisasa katika kuboresha mapato vile vile kulinda mazingira.
Wakiongozwa Benson Muchiri, waliwahimiza wakulima kujitenga na mbinu za jadi za kupalilia mashamba, akisema zimekuwa zikichangia mazao duni.
Muchiri ambaye amekuwa akitumia chupa na mabomba ya maji yaliyorushwa kuandaa sehemu za kuotesha mbegu kabla ya upanzi, amesema mbinu hiyo inasaidia kuokoa matumizi ya ardhi ipasavyo, sawa na kuhifadhi mazingira.
“Ninataka kuonyesha wakulima jinsi ya kufanya kilimo cha mjini, sio lazima uwe na kipande kikubwa cha ardhi ndio ufanye ukulima hasa kilimo cha mboga, ukiangalia vile vitu tulivyotumia hapa ni vile ambavyo ni kero, ukiangalia tuna chupa za plastiki ambazo tumezitumia, kile ambacho kinachafua mazingira hicho ndio tunahimiza mkulima badala ya hicho kitu kipotee wacha kiwe faida kwako”,alisema Muchiri.
Zaidi ya washirika 200 wanahudhuria maonyesho hayo ambayo yanaanza rasmi Jumatano 3 Septemba 2025, na kukamilika Jumapili 7 Septemba 2025.
Taarifa ya Joseph Jira
Business
Wafanyibiashara wa mitumba eneo la Diani wafunga biashara zao
Wafanyibiashara wa mitumba katika soko la Diani, kaunti ya Kwale, wamelazimika kufunga biashara zao kutokana na kudorora kwa shughuli za kibiashara katika kipindi hiki cha msimu wa watalii wachache na mvua zinazoendelea kushuhudiwa katika eneo hilo.
Wafanyabiashara hao wanasema idadi ya wanunuzi imepungua kwa kiasi kikubwa, hali iliyosababisha nguo nyingi kukosa soko.
Kulingana na wafanyibiashara hao wanategemea zaidi watalii wa ndani na nje na kutokana na msimu huu kuwa uko uko chini wateja wamepungua hali inayofanya maisha kuwa mgumu.
Wanasema wamelazimika kutupa baadhi ya nguo kwani zimesalia sokoni kwa muda mrefu hadi zingingine kuharibika, jambo ambalo limepelekea kupata hasara kubwa.
Aidha, wameongeza kuwa bei ya nguo za mitumba imeendelea kupanda ambapo wananunua ngunia moja kwa shilingi elfu 40 huku mauzo yakizidi kushuka.
“ Biashara imedorora sai kwani hakuna wateja ikizingatiwa kuwa tunategemea sana watalii na sasa hakuna wageni hata imetulazimu kutupa nguo kwani ngigi zimeharibika baada ya kukaa kwa mda mrefu bila kununuliwa”.
Taarifa ya Pauline Mwango
Business
Mamlaka ya AFA yahimiza upanzi wa mkorosho
Mamlaka ya Kilimo na Chakula nchini AFA, imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha taifa linaboresha mazao yake na kuchangia uzalishaji wa chakula nchini.
Hatua hii imechangia zaidi na mikakati endelevu ya kuwawezesha wakulima kufahamu mipango endelevu ya uimarishaji wa Kilimo cha sasa na kwa kuzingatia utumiaji wa mifumo bora ya kilimo.
Mamlaka hiyo ambapo inaendeleza kampeni ya kuhamisha wakulima kuhusu umuhimu wa kilimo cha Korosho imesisitiza haja ya ujumuishaji wa wakulima, wawekezaji na wadau mbalimbali ili kupiga jeki sekta ya Kilimo huku ikiahidi kuendeleza hamasa kwa jamii za kaunti za Pwani kuhusu kilimo cha korosho na utafutaji wa soko huru.
Katika Kongamano la kitaifa lililoandaliwa katika kaunti ya Kwale, Mamlaka hiyo iliwapa wakulima kutoka kaunti sita za Pwani miche ya mikorosho elfu mia moja katika juhudi za kukuza kilimo cha zao hilo nchini.
Katibu katika Idara ya Kilimo nchini Paul Kiprono, alisema mpango huo unalenga kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wa korosho na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Kiprono alitoa wito kwa serikali za kaunti pamoja na wadau wa sekta ya kilimo kushirikiana kwa karibu ili kuboresha kilimo cha korosho.
“Kenya ilikuwa ikiongoza katika zao la mkorosho katika miaka ya 1990 lakini kutokana na changamoto za kibiashara zao hilo lilishuka katika masoko ya kimataifa kutokana na ukosefu wa kuwekezaji kwa wakulima lakini sasa tumeanza kupiga hatua kwani tunazalisha zaidi ya tan elfu 9 za korosho”, alisema Rono.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa AFA, Cornelly Serem, alisema mamlaka hiyo imejizatiti kuboresha kilimo cha korosho kupitia utoaji wa miche bora na mafunzo kwa wakulima ili kuongeza tija.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

