News
Serikali ya kaunti ya Kilifi yaagizwa kusitisha utekelezaji wa bima ya matibabu
Mahakama ya Malindi kaunti ya Kilifi imetoa amri ya kusitishwa kwa utekelezwaji wa bima ya matibabu ambayo inapeanwa na serikali ya kaunti ya Kilifi.
Hii ni baada ya watu wawili kufikisha kesi mbele ya mahakama hiyo wakilalamikia namna harakati za kumtafuta mkandarasi wa bima hiyo zilivyofanywa.
Walalamishi hao Dishan Joel Mwanyumba na Edward Aranga wanasema shughuli hiyo haikufanywa kwa uwazi na aliyekabidhiwa kandarasi hiyo alikuwa amechaguliwa kabla ya kutangazwa kwa kandarasi hiyo.

picha kwa hisani/Mahakama ya Malindi
Kupitia wakili wao Omayo Aranga walalamishi hao wanasema kandarasi hiyo ya zaidi ya shilingi milioni 500 imekuwa na vigezo vigumu ambavyo vinafungia nje kampuni nyingi hasa kigezo cha malipo ya zaidi ya shilingi bilioni 2 katika mwaka wa fedha wa 2023 kwa kampuni ambazo zilituma maombi ili kupata kandarasi hiyo.
News
Mahakama ya Kilifi yawatupa gerezani washtakiwa zaidi ya 10
Mahakama ya Kilifi imetoa hukumu kwa washtakiwa zaidi ya 10 waliowasilishwa Mahakamani wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwemo kesi za unajisi na makosa ya jinai.
Katika vikao vya Mahakama siku ya Jumatano tarehe 3 June 2026, Hakimu Ivy Wasike ametoa hukumu hizo kwa watuhumiwa hao huku wengine wakifungwa kwa zaidi ya miaka 30 gerezani.
Simon Ngala, Aliwali Ali Mwalimu, Christopher Buru, miongoni mwa wengine zaidi ya 10 walifikishwa katika Mahakama ya Kilifi na kuhukumiwa kufuatia mashtaka mbalimbali yanayowakabili ikiwemo mashtaka ya unajisi na makosa ya jinai.
Hakimu wa Mahakama ya Kilifi Ivy Wasike, alimhukumu kifungo cha miaka 30 gerezani Simon Ngala baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi mtoto wa miaka 13 kisha akamtorosha kwao kwa kipindi cha mwezi mzima.
Mwengine ni Aliwali Ali Mwalimu, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 25 kufuatia mashtaka ya kumpachika ujauzito mtoto wa miaka 13 licha ya kuomba msamaha Mahakamani.
Wakati wa kutoa hukumu hizo, Hakimu Wasike alisikitishwa na kukithiri kwa visa vya watoto kupotea na kisha kunajisiwa katika kaunti ya Kilifi.
Kiongozi wa mashtaka katika Mahakama hiyo Nancy Njeru alipinga vikali ombi lililowasilishwa Mahakama la kutaka washtakiwa wasamehewe, kwanin wengine walidai kwamba walishirika makosa hayo bila kukusudia, akisema hukumu hizo zitakuwa funzo kwa watu wenye hulka hizo katika jamii.
Mbali na hukumu za kesi za unajisi, Christopher Buru alihukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani akikabiliwa na mashtaka ya wizi baada ya kupatikana na hatia ya kutumia pesa za mlalamishi Saumu Nyevu aliyekuwa akimtumia pesa alipokuwa akifanya kazi katika milki za kiarabu, kosa lililomchukiza zaidi Hakimu Wasike.
Taarifa ya Teclar Yeri
News
Washukiwa 5 wa uhalifu wanazuiliwa na polisi Likoni
Maafisa wa polisi katika eneo bunge la Likoni kaunti ya Mombasa wanawazuiliwa washukiwa 5 wa uhalifu waliokamatwa katika oparesheni iliyofanyika maeneo ya Duduz na Bufallo siku ya Jumatatu tarehe mosi Juni 2026.
Washukiwa waliokamatwa ni Brian Musa mwenye umri wa miaka 24, Abubakar Mahasi wa umri wa miaka 20, Juma Kassim mwenye umri wa miaka 16, Omar Gobeko maarufu Mboga mwenye umri wa miaka 19 na Jackson Mwambu mwenye umri wa miaka 26.
Msako huo uliongozwa na mkuu wa kituo cha polisi cha Shelly Beach pamoja na kikosi cha maafisa wa polisi.
Maafisa wa Polisi wamesema mshukiwa Brian Musa anakabiliwa na tuhuma za maandalizi ya kutenda kosa la jinai, huku Ababakar Mahasi, Juma Kassim na Omar Gobeko wakihusishwa na tuhuma za wizi wa mabavu.
Mshukiwa mwengine Jackson Mwambu anahusishwa na tuhuma za kupatikana na mali ya serikali kinyume cha sheria.
Katika oparesheni hiyo, maafisa wa polisi walifanikiwa kupata vielelezo mbali mbali ikiwemo panga tatu pamoja na koti la jeshi la KDF.
Taarifa ya Joseph Jira

