News
Serikali yawatahadharisha wakenya dhidi ya Ebola
Mkuu wa mawaziri nchini Musalia Mudavadi amewataka wakenya kuzingatia taratibu zilizotolewa na Wizara ya afya nchini kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Ebola katika nchi jirani ya Uganda.
Mudavadi amesema kwamba kama vile wakenya walivyofanya wakati wa janga la COVID-19, wanapaswa kuwa makini ili kuilinda nchi dhidi ya virusi vya Ebola.
Amesema kuwa ingawa hadi sasa hakuna kisa kilichoripotiwa nchini, uzembe unaweza kuliingiza taifa katika matatizo, akisisitiza kuzingatiwa kwa taratibu zote za kiafya zilizotolewa na Wizara ya Afya nchini dhidi ya virusi hivyo hatari na ambavyo vinasambaa kwa kasi.
Taasisi ya afya ya umoja wa afrika imesema nchi kumi za Afrika ziko katika hatari ya kuathiriwa na ugonjwa wa virusi vya Ebola, mbali na DRC na Uganda.
Kenya ilithibitisha kuwa visa vyote vinavyoshukiwa vya Ebola vilivyogunduliwa kupitia mfumo wake ulioimarishwa wa ufuatiliaji vilipatikana kuwa hasi, huku nchi ikiendelea kuimarisha uchunguzi mipakani na maandalizi ya dharura kufuatia mlipuko wa kikanda katika nchi jirani.
Waziri wa Afya nchini Aden Duale siku ya Ijumaa wiki jana alisema kuwa serikali imeongeza ufuatiliaji katika maeneo yote ya kuingia nchini lakini akawahakikishia wananchi kuwa hakuna maambukizi yaliyothibitishwa yaliyorekodiwa.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Mahakama ya Kilifi imehairisha kesi ya unyakuzi wa ardhi Kilifi
Mahakama ya Kilifi imehairisha kesi inayomhusu mshukiwa wa unyakuzi wa ardhi ya thamani ya shilingi milioni 165 hadi tarehe 29 mwezi Mei mwaka huu.
Armando Tanzini ambaye ni raia wa Italia pamoja na wenzake ambao hakuwa Mahakamani wanadaiwa kunyakua ardhi ya nambari Chembe-Kibabamshe/408, mali ya marehemu Kitsao Mashobo Nyaki.
Katika kesi hiyo, Kiongozi wa mashtaka ya umma Ridhwan Mohammed aliieleza Mahakama kwamba mnamo mwezi Machi mwaka 1994, washukiwa hao walifanya usajili wa ardhi hiyo katika ofisi za usajili wa ardhi mjini Kilifi wakijifanya kuwa wameuziwa ardhi hiyo.
Mahakama ilimuachilia Armando kwa dhamana ya shilingi laki 2 pesa tasilimu na Mahakama ikaagiza kuzuiliwa kwa cheti chake cha usafiri (passport) ili kupata muda wa kuwaleta washukiwa wengine Mahakamani
Katika kikao cha siku ya Jumatatu tarehe 25 mwezi Mei mwaka huu Mahakamani, Armando aliomba Mahakama kumrudishia cheti chake cha usafiri baada ya washukiwa wengine kukosa kufika mahakamani tangu kesi hiyo ianze, japo Mahakama ikasengeze kesi hiyo hadi tarehe 29 mwezi huu.
News
Viongozi wakosolewa kwa kutopambana na Mihadarati Pwani
Viongozi wa Pwani wamekosolewa kwa kulifumbia macho suala la ulanguzi wa dawa za kulevya lililosababisha vijana wengi kuangamia kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.
Kulingana na Mkereketwa wa masuala ya kisiasa mjini Malindi Athman Ali Said, viongozi hao wameshindwa kulizungumzia suala tata la Dawa za kulevya ambalo limekithiri katika eneo la Pwani.
Said alisema wakati wa ziara ya rais Ruto hapa Pwani, viongozi ambapo walichaguliwa kupigania maslahi ya jamii walionekana kukwepa kulizungumzia suala hilo na kuangazia masuala ya kisiasa na ajenda zao binafsi za siasa za uchaguzi mkuu ujao.
“Tulichokishuhudia wakati wa ziara ya rais hasa kaunti ya Kilifi ilikuwa ni ahadi na siasa za uchaguzi mkuu ujao, huku viongozi wa Pwani wanaotegemewa na wananchi kama wawakilishi wao wakiangazia maslahi yao. Hali hii haitakuwa rahisi kwa jinamizi la Mihadarati kukomeshwa katika ukanda wa Pwani”, alisema Said.
Kwa upande wake Mwanaharakati wa kupambana na Mihadarati kanda ya Pwani Famau Mohammed Famau alisema kuna haja ya viongozi wa Pwani kuliangazia kwa kina janga la Mihadarati ili likomeshwe.
“Ingekuwa ni vyema rais angegusia suala la dawa za kulevya na vile vile akatuoa muongozo kwa wale ambao wanapambana na madawa haya kwamba wafanye nini ili kuzuia madawa ya kulevya yasiendelee katika mji wetu wa Malindi na Kilifi kaunti”, alisema Fahamu

