Business
Bei ya mafuta ya Petroli, Dizeli na Taa yapanda
Huenda wakenya wakagharamika zaidi katika kumudu gharama ya maisha kutokana na ongezeko la bei ya mafuta ya Petroli, Dizeli na Taa mtawalia.
Hii ni kutokana na bei mpya iliyotolewa na Mamlaka ya kudhibiti Kawi na mafuta ya Petroli nchini EPRA kwani bei ya mafuta ya Petroli imeongezeka kwa shilingi 8.99, mafuta ya Dizeli kwa shilingi 8.67 na mafuta ya taa kwa shilingi 9.55 kwa lita.
Kulingana na EPRA, bei hiyo mpya itatumika kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi Agosti 14, ambapo bei ya mafuta ya Petroli katika jiji la Nairobi itauzwa kwa shilingi 186.31, Diseli kwa shilingi 171.58 na mafuta ya taa kwa shilingi 156.58.
Katika jiji la Mombasa bei hiyo mpya ya mafuta itauzwa kwa shilingi 183.02, mafuta ya Dizeli yatauzwa kwa shilingi 168.30 na mafuta ya taa yatauzwa kwa shilingi 153.29 kwa lita katika kipindi cha siku 30.
Hata hivyo katika kaunti ya Kilifi bei hiyo ya mafuta iko tafauti kwa sasa mafuta ya Petroli yatauzwa kwa shilingi 183.88, mafuta ya Dizeli yakiuzwa kwa shilingi 169.16 na matufa ya taa yatauzwa kwa shilingi 153.29 kwa lita.
Kulingana na taarifa kutoka EPRA, bei hiyo mpya mafuta imetoka na kupanda kwa bei ya mali ghafi kwa asilimia 6.45 ambayo ni Dola za Marekani 590.24 kwa “Cubic metre” kwenye mafuta ya Petroli mwezi Mei mwaka huu.
Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka hiyo Daniel Bargoria alisema japo bei hiyo huenda ikashuka iwapo soko huru la mafuta litapunguza bei ya mali ghafi ambayo imechangiwa na mizozo ya kivita katika mataifa yanayopigana ambayo na yamekuwa yanazalisha mafuta.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
Business
Bei za mafuta kuongezeka katikati ya mwezi aprili
Kenya sasa inakabiliwa na hatari ya kupanda kwa bei za mafuta, huku mgogoro unaoendelea mashariki ya Kati ukianza kuathiri bei nchini.
Serikali sasa imeonya kuwa kufikia katikati ya mwezi Aprili, bei za mafuta huenda zikapanda ikionya kuwa ongezeko la bei ya mafuta kwa sasa haliwezi kuepukika kufuatia kupanda kwa bei za mafuta kimataifa.
Waziri wa hazina kuu ya kitaifa John Mbadi aliwahakikishia wakenya kuwa hakuna cha kuhofia kwani wameweka mikakati kupunguza athari zake.
Ili kupunguza athari za bei za mafuta kuongezeka, serikali ilisema itatumia shilingi bilioni 17 kutoka mfuko wa ada ya uwekezaji wa mafuta kusaidia kudhibiti bei kwa mda wa miezi 3 ijayo.
Kwa sasa serikali inasema kuna akiba ya kutosha ya mafuta na shehena zaidi zinatarajiwa nchini hivi karibuni.
Taarifa ya Joseph Jira
Business
KPA yaimarisha usafirishaji wa makasha na kampeni za kimataifa
Halmashauri ya bandari nchini (KPA), imeimarisha ushirikiano wake na kampuni ya kimataifa ya usafirishaji kwa njia ya bahari, Maersk, katika juhudi za kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo katika eneo la Afrika Mashariki.
Makubaliano hayo yameafikiwa katika mkutano uliofanyika katika makao makuu ya KPA jijini Mombasa ambapo Mkurugenzi wa Maersk Kanda ya Afrika Mashariki, Tito Okuku, alieleza kuwa kampuni hiyo ina nia ya kupanua shughuli zake zaidi nchini na katika eneo la Afrika Mashariki kwa ujumla.
Moja ya maeneo yatakayopata kipaumbele ni kuimarisha matumizi ya Kituo cha Makontena cha ndani cha Naivasha kinachotazamwa kama kitovu muhimu katika kushughulikia usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka Kenya kwenda masoko ya kimataifa, huku kikitoa njia ya haraka na ya kuaminika kwa wauzaji kufikia masoko ya kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa KPA, Nahodha William Ruto, alieleza kukubaliana na hatua hiyo akisema ni wakati mwafaka kwa pande zote mbili kuimarisha ushirikiano huo.
Aidha alibainisha kuwa Bandari ya Mombasa pamoja na vituo vyake vya ndani vinaendelea kushuhudia ongezeko la shehena, na akahakikishia kuwa KPA iko tayari kushughulikia mahitaji yanayoongezeka kupitia maboresho ya miundombinu na huduma.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

