News
Kaunti ya Kilifi yajitenga na shutma za Aisha Jumwa
Serikali ya kaunti ya Kilifi imejitenga na vurugu zilizoshuhudiwa wakati wa mazishi ya Afisa wa kaunti katika eneo la Msabaha wadi ya Ganda eneo bunge la Malindi siku ya Jumatatu.
Akizungumza na vyombo vya habari, Naibu gavana wa Kilifi Flora Mbetsa Chibule, alidai kwamba wanasiasa wenye malengo fiche walitumia hafla ya mazishi na kutangaza semi za uongo kuhusu msaada wa kaunti kwa familia ya mwendazake.
Chibule alitangulia kwa kuomba msamaha kwa familia ya marehemu na kukariri kuwa serikali ya kaunti kupitia gavana Gedion Mung’aro awali iliwasiliana na familia kuhusu namna ya kuipa msaada, japo haukuwekwa hadharani.
Wakati huo huo Chibule alidokeza kwamba gavana Mung’aro binasfi alitoa msaada wake wa fedha kwa familia ya marehemu.
“Huyu ni mfanyakazi wa serikali ya kaunti mbali na mstahiki gavana wetu, idara ya ugatuzi na utekelezaji ilichangia kwa mambo hayo ya mazishi, alipokuwa na anaenda kuangaliwa maisha yake kule Moshi mustahiki gavana mwenyewe alitoa nusu milioni kumsaidi Baloteli(marehemu), nilikwenda pale tukaramuka(kuomboleza) tukasema mama madamu unahii shahada tutakutafutia nafasi katika serikali ya kaunti”, alisema Chibule.
Vile vile naibu gavana huyo aliwapa changamoto viongozi wa siasa kuheshimu hafla za mazishi na kupunguza siasa hasa wanapoalikwa katika hafla hizo.
“Jana Msabaha mfanyakazi wetu shupavu almaarufu Baloteli nikwamasikitiko makuu ya kwamba matokeo ya mazishi yale yalikwenda vile yalivyo sisi kama serikali ya kaunti tunaomba msamaha kwa familia, kwa mama Mbeyu tusamehe kwa jinsi shughuli ilivyokuwa, viongozi wenzangu tafadhali mazishi yaheshimiwe”, alisistiza naibu gavana Chibule.
Katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya kitaifa ya barabara Aisha Jumwa alitoa changamoto kwa viongozi wa kaunti ya Kilifi kumpa ajira mke wa Marehemu kauli ambayo iliibua hisia miongoni mwa viongozi na kusababisha rabsha.
“Nimesikiza viongozi wa kaunti hapa mmoja mpaka wa mwisho wakizungumza, sikupata hata mmoja mwenye huruma aseme Baloteli ametumikia kaunti na hivi amefariki mkewe Maurine jumatatu au jumanne ako kazini, sikusikia, lakini mimi nilikuwa nimevipanga, mmkuja matangani na kama mmempangia simzunguze kila mtu asikie, lakini kwa sababu havikuzungumiziwa nimevipatia wiki moja kama hatapata kazi nitarejea hapa maana mwanijua mimi ni mtu wa matendo”, alisema Jumwa.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Polisi wanachunguza tukio la wizi dhidi ya raia wa kigeni
Maafisa wa Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza tukio la wizi dhidi ya mtalii wa kigeni lililotokea katika eneo la Nyali
Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, mtalii huyo mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni raia wa Marekani, anadai kulaghaiwa na kisha kushambuliwa na kundi la wanaume aliyokutana nao muda mfupi kabla ya tukio.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba mnamo mwezi Aprili 9 mwaka huu, raia huyo wa kigeni akiwa katika mkahawa mmoja eneo la Nyali jijini Mombasa, alikutana na mwanaume aliyejitambulisha kama Alex, ambaye alimshawishi kuelekea katika nyumba ya Airbnb iliyoko karibu na mkahawa huo.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kwamba alipofika katika chumba hicho, alikumbana na wanaume wengine watano waliokuwa wakimsubiri ambapo mlango ulifungwa na kisha akashambuliwa na kulazimishwa kutoa pesa na vitu vya thamani.
Wahalifu hao walitoroka na mali mbalimbali ikiwemo simu ya rununu, kompyuta mpakato (laptop), fedha taslimu pamoja na fedha za kigeni na pia walifanikiwa kutoa pesa kutoka kwenye kadi zake za benki kwa njia ya udanganyifu.
Maafisa wa polisi kutoka Bamburi kwa kushirikiana na maafisa wa upelelezi wa DCI Nyali walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, ingawa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa wala mali iliyopatikana.
Kesi hiyo imewekwa chini ya uchunguzi zaidi huku juhudi zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Polisi eneo la Likoni-Mombasa inachunguza kifo cha mwanamke
Idara ya usalama eneo la Likoni kaunti ya Mombasa imesema inachunguza kifo cha mwanamke mmoja aliyefariki katika mtaa wa senti kumi.
Mkuu wa polisi wa Likoni Joseph Mutungi alisema mwanamke huyo anadaiwa kupoteza maisha wakati wakiwa nyumbani kwa mwanamme anayesemekana kuwa mchumba wake.
Taarifa za awali ziliarifu kuwa marehemu alikuwa mgonjwa na anadaiwa alifika hospitalini kusaka matibabu japo hakupata huduma na kurejea nyumbani bila kutibiwa.
Inasemekana baadaye mchumba wake alioondoka kwenda kazini na kumwacha chini ya uangalizi wa mwanamke mwengine katika ploti hiyo.
Hali yake inadaiwa kuzorota na hatimaye kuaga dunia.
Maafisa wa usalama walisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Coast general kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

