News
Mahakama Kuu yasitisha mpango wa Marekani na Kenya wa kuanzisha kituo cha karantini cha Ebola
Mahakama Kuu nchini imesitisha kwa muda mpango wa serikali ya Marekani na Kenya wa kuanzisha kituo cha karantini cha Ebola humu nchini.
Jaji wa Mahakama hiyo, Patricia Nyaundi, ameagiza kusitishwa kwa muda kwa utekelezaji wa makubaliano hayo hadi pale kesi iliyowasilishwa Mahakamani itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Katika uamuzi wake, Jaji Nyaundi alisema Kenya pia hairuhusiwi kupokea mtu yeyote aliyekumbana na Ebola au aliyeambukizwa ugonjwa huo chini ya mpango huo hadi kesi hiyo itakapomalizika.
Shirika la kutetea haki za kiraia la Katiba Institute liliwasilisha kesi hiyo mahakamani likipinga mpango huo siku hiyo hiyo ulipotangazwa.
Shirika hilo limesema kuanzishwa kwa kituo hicho kwa siri na bila ushirikishwaji wa umma kunazua maswali mengi kuhusu haki za maisha, afya, uwajibikaji wa serikali na usimamizi wa bunge.
Kabla ya kesi hiyo kuwasilishwa Mahakamani, Serikali ya Marekani kupitia Rais Donald Trump ilikuwa imekubaliana na Kenya na kutangaza mpango wa kuwahifadhi kwa muda raia wake waliokumbana na virusi vya Ebola nchini Kenya.
Hatua hii ililenga kuzuia ugonjwa huo kuingia katika ardhi ya Marekani, ambapo sasa mpango huo umekumbana na kikwazo kikubwa baada ya Mahakama kuu nchini kusimamisha kwa muda mpango huo.
Kwa mujibu wa Ikulu ya White House, raia wa Marekani waliokuwa katika maeneo yenye mlipuko wa Ebola lakini hawajaonyesha dalili za ugonjwa huo walitarajiwa kuwekwa katika kituo maalum cha karantini katika Kambi ya Anga ya Laikipia mjini Nanyuki.
Maafisa wa utawala wa Marekani walikuwa wamesema wale ambao wangepata dalili za Ebola hawangerejeshwa Marekani, bali wangepelekwa katika nchi nyingine kwa matibabu ya juu zaidi.
Hatua hiyo ilionekana kuwa mabadiliko makubwa ya sera ikilinganishwa na milipuko ya Ebola iliyopita ambapo wagonjwa Wamarekani waliruhusiwa kurejeshwa nyumbani kwa matibabu.
Lengo la mpango huo lilikuwa kuhakikisha hakuna kisa cha Ebola kinachoingia nchini Marekani.
News
Mahakama ya Kilifi yaagiza mshukiwa wa mauaji kuzuiliwa kwa siku 21
Mahakama ya Kilifi imeagiza kuzuiliwa rumande kwa siku 21 mwanamke mmoja anayekabiliwa na shtaka la kumuuwa mwanawe kwa kumzika akiwa hai.
Hakimu wa Mahakama hiyo Charles Obulutsa ametoa agizo hilo baada ya upande wa mashtaka kuiomba Mahakama kumpa muda zaidi ili kuwawezesha maafisa wa upelelezi wa kesi hiyo kukamilisha uchunguzi wao.
Kulingana na upande wa mashtaka ukiongozwa na Nancy Njeru ulieleza Mahakama kwamba mtoto huyo alikuwa ameishi siku mbili baada ya kuzuiliwa.
Mahakama imeelezwa zaidi kwamba kabla ya mshukiwa kumzika mtoto huyo akiwa hai, ni lazima mwanamke huyo alikuwa na tatizo ndiposa upande wa mashtaka uanitaji muda zaidi kwa kufanya uchunguzi sawa na kumhoji mshukiwa.
Mshukiwa Maua Karisa anadaiwa kumzaa mwanawe tarehe 24 Mei 2026, na kutekeleza kitendo hicho tarehe 26 Mei 2026 katika eneo la Matsangoni kaunti ya Kilifi.
Kesi hiyo itatajwa tarehe 22 mwezi Juni mwaka huu.
Taarifa ya Tecla Yeri
News
Pengo katika uhamasishaji wa afya ya uzazi kilifi
Idadi kubwa ya wanawake na wasichana katika kaunti ya Kilifi bado hawajahamasishwa vilivyo kuhusu masuala ya afya ya uzazi na haki yao ya kupata huduma bora ya afya hasa katika maeneo ya mashinani.
Katika kikao ambacho kiliongozwa na shirika la Timiza Youth Initiative kwenye ukumbi wa Kibaoni mjini Kilifi kaunti ya Kilifi na kuhudhuriwa na vijana, wahudumu wa afya na wadau mbalimbali, ilibainika kuwa afya ya wanawake haijakumbatiwa vilivyo katika jamii hali ambayo imekuwa ikifanya wengi wao kupitia changamoto nyingi na hata kufariki dunia wakati wa ujauzito na wanapojifungua.
Akizungumzia hilo Brian Mundia ambaye ni mwenyekiti wa shirika hilo alisema wasichana wenye umri mdogo pia hawajaelimishwa vya kutosha kuhusu athari ya kupanga uzazi na kuavya mimba.
Mundia pia alisema vijana wengi wanaogopa kufika katika vituo vya afya kupata ushauri kutokana na hali ya unyanyapaa .
Kwa upande wake Doris Waithira Mzee wa kijiji eneo la Mnarani na ambaye pia anatoa ushauri nasaha kwa wanarika alisema akina mama wengi hawaendi hospitalini kujifungua hali ambayo pia huwa inahatarisha afya ya mtoto.
Kwa pamoja walieleza changamoto zilizopo katika kuwafikia wanawake walioko mashinani ili kutoa hamasa na kutoa wito kwa mashirika na serikali kupitia idara ya afya kushirikiana ili kuhakikisha masuala ya afya ya uzazi na afya ya mama katika jamii inakumbatiwa vilivyo.
Taarifa ya Janet Mumbi

