News
Mahakama ya Mombasa Kusikiliza Kesi ya Mauaji ya Afisa wa IEBC
Mahakama kuu ya Mombasa imeanza kuskiliza kesi ya mauaji ya aliyekuwa Kaimu Meneja wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC katika kaunti ya Kilifi Aisha Akinyi Abubakar.
Washtakiwa katika kesi hiyo, Joseph Sunday Otieno maarufu Brian Shikuku na Brian Templer Oyare wanakabiliwa na tuhuma za mauaji ya afisa huyo nyumbani kwake katika mtaa wa Utange eneo bunge la Kisauni katika kaunti ya Mombasa mnamo mwezi Januari tarehe 5 mwaka huu.
Wawili hao pia walishtakiwa kwa kosa la kumpiga na kumjeruhi Mwanawe Marehemu na kutoweka na vifaa vya kieletroniki ikiwemo simu na vifaa vya IEBC, nyumbani kwao wakati wa tukio hilo.
Jaji Wendy Micheni ameanza kusikiliza kesi hiyo baada ya vipimo vya kiafya kutoka kwa madaktari kubaini kwamba washukiwa hao wawili wana akili timamu, hii ni baada ya Mahakama hapo awali kuagiza washukiwa hao wafanyiwe vipimo vya afya akili.
Oyare na Otieno wataendelea kufuatilia vikao vya kesi hiyo wakiwa rumande baada ya Mahakama kuwanyima dhamana kutokana na mashtaka yanayowakabili.
Kesi hiyo itaendelea kesho katika Mahakama hiyo.
News
Sakata ya mafuta yaathiri sekta ya uchukuzi nchini
Huenda watumizi wa magari ya uchukuzi wa umma, wahudumu wa tuktuk na bodaboda wakalazimika kuongeza nauli kwa abiria kutokana na changamoto za ukosefu wa mafuta nchini na kuathiri zaidi shughuli za uchukuzi.
Hatua hii imetakana na changamoto za uhaba wa mafuta nchini baada ya kuibuka kwa sataka ya uagizaji wa mafuta ghushi kupitia bandari ya Mombasa.
Kulingana na serikali kupitia Wizara ya Kawi, sakata hiyo ya shilingi bilioni 12 ilikuwa imelata tani elfu 60 za mafuta ya petroli kinyume cha sheria pamoja na mipango ya serikali ya uagizaji mafuta wa serikali kwa serikali yaani G to G.
Sakata hii imepelekea Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya kudhibiti kawi na bei za mafuta nchini EPRA Daniel Kiptoo, Katibu katika Idara ya petroli nchini Mohammed Liban na mkurugenzi wa Kampuni ya Kenya Pipeline Joe Sang kujiuzulu.
Kujiuluzu kwao kumetokana na kukamatwa na maafisa wa idara ya upelelezi wa jinai nchini DCI, kwa ushirikiano na Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC baada ya kutilia shaka zabuni iliyopewa kampuni binafsi ya One Petroleum Limited inayomilikwa na mfanyibiashara mashuhuri jijini Mombasa.

Wahudumu wa sekta ya bodaboda wakikabiliwa na changamoto za uhaba wa mafuta ya Petroli
Siku ya Jumanne, Waziri wa Kawi nchini Opiyo Wandanyi alifanya kikao na wakurugenzi wa kampuni za mafuta nchini na kuagiza shehena ya mafuta katika bandari ya Mombasa kurejeshwa kwani serikali haitambua shehena hiyo.
“Wahusika wa sakata hiyo walikuwa na njama ya kuongeza bei ya mafuta nchini kwa shilingi 14 zaidi kwa lita wakitumia nafasi ya vita vinavyoendelea kati ya Iran na Marekani na Israel, hiyo hatuta kubali”, alisema Wandayi.
Hatua hiyo ilikuwa inalenga pia kukwepa mpango wa serikali wa uagizaji mafuta kutoka mataifa ya miliki za kiarabu wa serikali kwa serikali yaani G to Go, akisema wahusika wa sakata ya ufisadi ni lazima wachukuliwe hatua.
Itakumbukwa kwamba rais William Ruto hivi majuzi alidokeza kwamba wahusika wote wa sakata ya ufisadi kwenye sekta ya mafuta watachukuliwa hatua, akishililia kwamba serikali haitakubali ufisadi nchini, huku akikosa kuweka wazi hatma ya maafisa hao wakuu wa serikali.
“Hawa walaghai wa mambo ya mafuta watakipata, hawaweze kuhepa kwa sababu haiwezekani katika taifa letu la Kenya watu wanaone tuko na shida ya mashariki ya kati wanakuja kukoroga shida nyengine hapa Kenya, serikali itakabiliana kikamilifu na wafisadi”, alisema Rais Ruto.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Buriani Mama Dorothy Baya, 1947-2026
Mwili wa Mama Dorothy Baya Mweri ambaye ni Mama mzazi wa bunge wa Kilifi Kazkazini Owen Baya umetolewa katika makafani ya hospitali ya rufaa ya Kilifi kaunti ya Kilifi.
Mwili wa Mama Dorothy umefanyiwa ibada fupi ya wafu nje ya makafani ya hospitali hiyo ikiongozwa na viongozi wa kidini kisha wananchi wakapata fursa ya kuutazama mwili ili kutoa heshima yao ya mwisho kwa marehemu.
Viongozi mbalimbali wa kisiasa pia walikuwa na nafasi ya kumpa mkono wa buriani Mama Dorothy wakiongozwa na Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro na Mwenyekiti wa bodi ya hazina ya michezo na sanaa ambaye pia ni mgombea wa wadhfa wa useneta kaunti ya Kilifi Wakili George Kithi.
Viongozi wengine waliokuwepo kutoa heshima zao za mwisho kwa Marehemu ni pamoja Mbunge wa Ganze Kenneth Tungule, Mbunge wa Kaloleni Paul Katana, Mgombea wa wadhfa wa uwakilishi wa kike kaunti ya Kilifi Christine Zawadi, miongoni mwa wengine.
Msafara wa Marehemu baadaye ulielekea katika kijiji cha Dabaso eneo bunge la Kilifi Kazkani kaunti ya Kilifi kwa ibada ya misa ya wafu katika Kanisa la St Stephen Dabaso kabla ya halfa ya mazishi siku ya Jumatatu.

Msafara wa Marehemu Mama Dorothy Baya ukielekea katika kijiji cha Dabaso eneo bunge la Kilifi Kazkani kaunti ya Kilifi kwa hafla ya mazishi.
Marehemu amewaacha watoto 6, akiwemo Mbunge wa Kilifi Kazikazini ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa wengine bungeni Owen Baya, Askofu mkuu wa Kanisa la Kianglikana Dayosi ya Mombasa Alphonce Mwaro,Charity Mapenzi, Felix Mweri, Mercy Kadii na Catherine Harusi, pamoja na wajuu kadhaa.
Hata hivyo viongozi na wananchi wa tabaka mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria halfa ya mazishi ya Mama Dorothy itakayofanyika siku ya Jumatatu hapo kesho tarehe 6 mwezi Aprili mwaka huu katika kijiji cha Dabaso.
Mama Dorothy aliaga dunia tarehe 30 mwezi Machi, 2026.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

