Business
Serikali yachukua hatua za haraka kupunguza bei za mafuta
Mamlaka ya kudhibiti bei ya mafuta nchini EPRA imetangaza kupunguzwa kwa bei ya mafuta ya Petroli, Dizeli na Taa humu nchini.
Kaimu Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka hiyo Mhandisi Joseph Oketch katika taarifa aliyoitoa, ametangaza kupunguzwa kwa bei ya mafuta ya petroli kwa shilngi 9.37, mafuta ya Dizeli kwa shilingi 10.21 huku bei ya mafuta ya Taa ikisalia kama kawaida.
Oketch amesema hatua hiyo ni baada ya Hazina ya kitaifa kupunguza ushuru wa mafuta kwa asilimia 8 kutoka asilimia 13 ili kuchangia kupungua kwa gharama ya ununuzi wa mafuta baada serikali kutenga shilingi bilioni 6.5 za ruzuka ya mafuta.
Hatua hii imejiri mda mchache tu baada ya Mamlaka hiyo awali kutangaza bei ya mafuta ya Petroli kupanda kwa shilingi 28 kwa lita na mafuta ya Dizeli yakipanda kwa shilingi 40 kwa lita, hatua iliyosababisha viongozi wa upinzani kutishia kuitisha maandamano ya kitaifa kushinikiza kupunguzwa kwa bei hizo za mafuta nchini.
Hata hivyo katika taarifa ya Mamlaka ya EPRA, ilisema mafuta ya Petroli sasa yatauzwa kwa shilingi 197.60 kwa lita, huku mafuta ya Dizeli yakiungwa kwa shilingi 196.63 kwa lita na mafuta ya Taa yakisalia shilingi 152.78 kwa lita, katika jiji la Nairobi.
Mjini Mombasa, bei ya mafuta ya Petroli sasa itauzwa kwa shilingi 194.32, mafuta ya Dizeli yakiuzwa kwa shilingi 193.35 huku mafuta ya Taa yakiuzwa kwa shilingi 149.49 kwa lita na mjini Kilifi bei hiyo ya mafuta ikipungua na mafuta ya Petroli sasa yatauzwa kwa shilingi 195.18, mafuta ya Dizeli yakiuzwa kwa shilingi 194.22 huku mafuta ya Taa yakiuzwa kwa shilingi 150.36 kwa lita.
Hata hivyo Mamlaka hiyo imesema tangazo hilo limezingatia notisi ya kisheria nambari 70 na kwamba bei hiyo mpya ya mafuta inaanza kutekelezwa mara moja na itadumu kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi tarehe 14 mwezi Mei mwaka huu.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
Business
Mamlaka ya AFA yahimiza upanzi wa mkorosho
Mamlaka ya Kilimo na Chakula nchini AFA, imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha taifa linaboresha mazao yake na kuchangia uzalishaji wa chakula nchini.
Hatua hii imechangia zaidi na mikakati endelevu ya kuwawezesha wakulima kufahamu mipango endelevu ya uimarishaji wa Kilimo cha sasa na kwa kuzingatia utumiaji wa mifumo bora ya kilimo.
Mamlaka hiyo ambapo inaendeleza kampeni ya kuhamisha wakulima kuhusu umuhimu wa kilimo cha Korosho imesisitiza haja ya ujumuishaji wa wakulima, wawekezaji na wadau mbalimbali ili kupiga jeki sekta ya Kilimo huku ikiahidi kuendeleza hamasa kwa jamii za kaunti za Pwani kuhusu kilimo cha korosho na utafutaji wa soko huru.
Katika Kongamano la kitaifa lililoandaliwa katika kaunti ya Kwale, Mamlaka hiyo iliwapa wakulima kutoka kaunti sita za Pwani miche ya mikorosho elfu mia moja katika juhudi za kukuza kilimo cha zao hilo nchini.
Katibu katika Idara ya Kilimo nchini Paul Kiprono, alisema mpango huo unalenga kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wa korosho na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Kiprono alitoa wito kwa serikali za kaunti pamoja na wadau wa sekta ya kilimo kushirikiana kwa karibu ili kuboresha kilimo cha korosho.
“Kenya ilikuwa ikiongoza katika zao la mkorosho katika miaka ya 1990 lakini kutokana na changamoto za kibiashara zao hilo lilishuka katika masoko ya kimataifa kutokana na ukosefu wa kuwekezaji kwa wakulima lakini sasa tumeanza kupiga hatua kwani tunazalisha zaidi ya tan elfu 9 za korosho”, alisema Rono.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa AFA, Cornelly Serem, alisema mamlaka hiyo imejizatiti kuboresha kilimo cha korosho kupitia utoaji wa miche bora na mafunzo kwa wakulima ili kuongeza tija.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
Business
Wafanyabiashara wanataka wachuuzi kuondolewa Sokoni, Kilifi
Wafanyabiashara wa soko la kwa Charo wa mae mjini kilifi kaunti ya Kilifi, wanaitaka serikali ya kaunti kuwaondoa wachuuzi wanaoendeleza biashara zao nje ya Soko hilo.
Wakiongozwa na Florence Kazungu, wafanyibiashara hao wanasema kuwa biashara imepungua kwani wateja wengi wananunua bidhaa nje ya soko hali inayofanya mapato yao kupungua.
Wamesema kuwa licha ya wao kulipa ushuru katika soko hilo, bidhaa zao zinasalia sokoni kutokana uhaba wa wateja hali inayowasababishia hasara kwani bidhaa nyingi huharibika.
Hata hivyo wanaitaka serikali ya kaunti kuingilia kati suala hili na kuwaondoa wachuuzi hao.
“Biashara iko chini wateja hawaingii sokoni kwa sababu wananunua bidhaa hapo nje ya soko hali inayotufanya tunasalia na bidhaa zetu hadi zinaharibika ili hali tunalipa ushuru, serikali inafaa iwatoe wachuuzi hao ili sisi nasi tuweze kupata riziki ya kila siku”. alisema Florence.
Taarifa ya Pauline Mwango

