News
Shambulio la Osotsi lazua wasiwasi kwa upinzani
Seneta wa Vihiga Godfrey Ososti anaendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Karen jijini Nairobi baada ya kusafirishwa kwa ndege jana Jumatano April 8 2026 kutoka mjini Kisumu, siku moja tu baada ya Naibu Kinara huyo wa Chama cha ODM, kuvamiwa na kundi la vijana waliojihami kwa silaha hatari mjini Kisumu.
Viongozi mbali mbali hasa kutoka upande wa upinzani nchini Kenya, wamekuwa wakitoa kauli kali za kushtumu shambulio hilo wakihoji nia na dhamira ya shambulio hilo.
Osotsi ni miongoni mwa Viongozi wanaoasi Chama cha Odm katika mrengo wa Linda Mwananchi, wakiongozwa na Seneta wa Nairobi ambaye pia ni Katibu wa chama hicho Edwin Sifuna.
Wakiongozwa na Knara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, walisema shambulio hilo dhidi ya seneta Osotsi huenda ni njama na vitisho kwa kusudi la kuzua uhasama baina ya jamii mbili za eneo la magharibi mwa nchi.
Kalonzo alisema viongozi wa kisiasa hasa wa upinzani wanafaa kupewa uhuru na mazingira salama ya kuuza sera zao za siasa sawa na viongozi wengine serikalini, huku akishinikiza serikali kuhakikisha wahuni hao wanakamatwa na kukabiliwa kisheria.
Kiongozi huyo wa upinzani aliongeza kusema, iwapo serikali haitachukua hatua za haraka basi watalazimika kumfungulia mashtaka Waziri wa usalama wa ndani Kichumba Murkomen na Katibu katika Wazira hiyo Raymond Omollo.

Viongozi wa kisiasa washutumu shambilio la kivamizi dhidi ya Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi
Kauli yake iliungwa mkono na Kinara wa chama cha DAP-Kenya Eugine Wamalwa ambaye alisema wahuni wamekuwa wakishambulia viongozi wa upinzani mara kwa mara jambo linalohatarisha usalama wa viongozi.
Katika kanda ya video iliyonaswa kwenye kamera za siri za CCTV siku ya Jumatano, kundi la vijana lilionekana likiingia kwenye mghahawa mmoja kisha kumshambulia na kumjeruhi seneta huyo.
Wakati huo huo Seneta wa Kakamega Bonny Khaluale aliitaka idara ya upelelezi nchini kuzamia suala la uvamizi dhidi ya viongozi unaotekelezwa na vijana wanaoonekana kukodishwa ili kuwanyamazisha wapinzani.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Polisi wanachunguza tukio la wizi dhidi ya raia wa kigeni
Maafisa wa Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza tukio la wizi dhidi ya mtalii wa kigeni lililotokea katika eneo la Nyali
Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, mtalii huyo mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni raia wa Marekani, anadai kulaghaiwa na kisha kushambuliwa na kundi la wanaume aliyokutana nao muda mfupi kabla ya tukio.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba mnamo mwezi Aprili 9 mwaka huu, raia huyo wa kigeni akiwa katika mkahawa mmoja eneo la Nyali jijini Mombasa, alikutana na mwanaume aliyejitambulisha kama Alex, ambaye alimshawishi kuelekea katika nyumba ya Airbnb iliyoko karibu na mkahawa huo.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kwamba alipofika katika chumba hicho, alikumbana na wanaume wengine watano waliokuwa wakimsubiri ambapo mlango ulifungwa na kisha akashambuliwa na kulazimishwa kutoa pesa na vitu vya thamani.
Wahalifu hao walitoroka na mali mbalimbali ikiwemo simu ya rununu, kompyuta mpakato (laptop), fedha taslimu pamoja na fedha za kigeni na pia walifanikiwa kutoa pesa kutoka kwenye kadi zake za benki kwa njia ya udanganyifu.
Maafisa wa polisi kutoka Bamburi kwa kushirikiana na maafisa wa upelelezi wa DCI Nyali walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, ingawa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa wala mali iliyopatikana.
Kesi hiyo imewekwa chini ya uchunguzi zaidi huku juhudi zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Polisi eneo la Likoni-Mombasa inachunguza kifo cha mwanamke
Idara ya usalama eneo la Likoni kaunti ya Mombasa imesema inachunguza kifo cha mwanamke mmoja aliyefariki katika mtaa wa senti kumi.
Mkuu wa polisi wa Likoni Joseph Mutungi alisema mwanamke huyo anadaiwa kupoteza maisha wakati wakiwa nyumbani kwa mwanamme anayesemekana kuwa mchumba wake.
Taarifa za awali ziliarifu kuwa marehemu alikuwa mgonjwa na anadaiwa alifika hospitalini kusaka matibabu japo hakupata huduma na kurejea nyumbani bila kutibiwa.
Inasemekana baadaye mchumba wake alioondoka kwenda kazini na kumwacha chini ya uangalizi wa mwanamke mwengine katika ploti hiyo.
Hali yake inadaiwa kuzorota na hatimaye kuaga dunia.
Maafisa wa usalama walisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Coast general kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

