News
JSC yamteua Jaji Mohammed Warsame kuwa Jaji wa Mahakama ya Upeo
Tume ya huduma ya Mahakama nchini (JSC) imemteua Jaji Mohammed Abdullahi Warsame kuwa Jaji wa Mahakama ya Upeo.
Mwenyekiti wa Tume hiyo ambaye pia ni Jaji mkuu nchini Martha Koome alisema jina la Jaji Warsame litawasilishwa kwa rais William Ruto ili kuteuliwa rasmi kwa kuambatana na Katiba na sheria nchini kisha kuliwasilisha bungeni kuidhinishwa rasmi.
Jaji Koome alisema Tume hiyo imezingatia masuala mbalimbali wakati wa mahojiano ikiwemo suala la uadilifu, uwajibikaji, usawa, hadhi ya kuwa jaji miongoni mwa masuala mengine kabla ya Tume hiyo kuridhia umuazi huo.
Jaji Warsame alikuwa miongoni mwa wakenya 5 waliotuma maombi ya kukuwa Jaji wa Mahakama ya upeo baada ya kifo cha Jaji Mohammed Ibrahim, Disemba mwaka 2025.

Mahojiano ya kutafuta nafasi Jaji wa Mahakama ya upeo katika Mahakama ya Milimani jijini Nairobi
Waliohojiwa katika nafasi hiyo ni pamoja na Jaji wa Mahakama kuu Katwa Kigen, na Francis Tuiyott pamoja na Jaji wa Mahakama kuu Joseph Sergon pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mamlaka huru ya usimamizi wa maafisa wa Polisi (IPOA) Anne Waceke Makori.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Wadau wa sekta ya uchukuzi wasitisha mgomo wao
Maafisa wa sekta ya uchukuzi wameahirisha mgomo wao baada ya mazungumzo yaliyoongozwa na Rais William Ruto katika ikulu ya Mombasa.
Maafisa hao wakiongozwa na rais wa Muungano wa wamiliki wa matatu Albert Karagacha wamesema kuwa mengi ya masuala waliokuwa nayo ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta nchini yameangaziwa kwa kina na rais Ruto.
Karagacha amewataka wahudumu wa sekta ya uchukuzi wa umma pamoja na wamiliki wa magari ya uchukuzi wa mizigo kuhakikisha wanarudisha magari yao barabarani, akisema masuala waliowasilisha kwa rais yameangaziwa
Akizungumza mda mfupi baada ya kufanya kikao na rais William Ruto mjini Mombasa, Karagacha amesema serikali imekuwa kiangazia kwa kina masuala mbali mbali yanayohusu sekta ya uchukuzi nchini.
Aidha amesema iwapo bado serikali itakuwa inajikokota katika kufanikisha masuala waliojadiliana basi wataitisha mazungumzo zaidi na Wizara husika ili kuafikiwa kwa ajenda zao huku akisema japo suala la mzozo wa mafuta sio jambo la Kenya pekee lakini taifa inawajibu wa kusaidia wananchi wake.
Wakati huo huo Karagacha amewataka wakenya kutoingiza siasa katika suala la kupanda kwa bei ya mafuta nchini.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Mshukiwa wa ulanguzi na usafirishaji wa watoto anyimwa dhamana
Mahakama ya Shanzu imemnyima dhamana mshukiwa wa ulanguzi wa watoto zaidi ya 20.
Mahakama imeagiza mshukiwa huyo kuzuiliwa rumande ili kuwawezesha maafisa wa polisi kukamilisha uchunguzi wao.
Mahakama imeelezwa kwamba mshukiwa huyo Almasi Rama Amos mwenye umri wa miaka 27 alikamatwa na maafisa wa upelelezi kutoka kitengo cha kupambana na ulanguzi wa binadamu na ulinzi wa watoto (AHTCPU) pamoja na maafisa wa idara ya upelelezi wa Jinai kutoka kaunti ya Mombasa.
Kukamatwa kwake kufuatia wiki kadhaa za uchunguzi kuhusu ripoti za unyanyasaji wa watoto zinazowalenga wasichana wadogo walio katika mazingira magumu.
Rama, anayetuhumiwa kwa kujihusisha na kundi linalodaiwa kuwa la ulanguzi wa watoto na dhulma za kingono na kufikishwa katika Mahakama ya Shanzu kufuatia operesheni ya kiusalama iliyoidhinishwa na maafisa hao.
Rama alipatikana katika mtaa wa Nguu Tatu eneo la Concordia katika kaunti ndogo ya Kisauni akiwa na watoto watatu wa kike.
Mahakama imeelezwa kuwa mshukiwa anadaiwa kuendesha “vituo vya uokoaji” katika kaunti za Mombasa na Kilifi kwa kujifanya kuwalea na kuwapa ushauri.
Kulingana na uchunguzi vituo hivyo vilikuwa vikitumika kama msingi wa dhulma za kingono na unyanyasaji wa watoto.
Alipokamatwa, mshukiwa aliwaongoza maafisa hadi kituo chengeni eneo la Ribe katika eneo bunge la Rabai, ambapo maafisa wa upelelezi waliwaokoa watoto 19 wa jinsia ya kike na kufikisha jumla ya waathiriwa waliookolewa kufikia ishirini na wawili (22).
Mbele ya Mahakama ya Shanzu tarehe 21 Mei, 2026, mshukiwa amekabiliwa na mfululizo wa mashtaka, ikiwemo unajisi, biashara ya watoto kwa madhumuni ya kuwadhulumu kingono pamoja na unyanyasaji wa watoto ambapo amekana mashtaka hayo.
Kesi hiyo imepangwa kutajwa Juni 8, 2026.
Taarifa ya Teclar Yeri

