News
Bei ya Mafuta yapandisha joto la kisiasa nchini
Mjadala kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli nchini Kenya unaendelea kushika kasi, huku wananchi wengi wakitaka maelezo ya kina kuhusu vigezo vinavyotumika kuongeza bei hizo karibu kila mwezi.
Wadau wengi wameonyesha wasiwasi wao kuhusu tofauti ya bei ya mafuta kati ya Kenya na mataifa jirani yasiyo na bandari kama Uganda, Rwanda na Burundi, hali ambayo imeibua maswali kuhusu mfumo wa uagizaji na usimamizi wa mafuta nchini.
Shinikizo hilo limechochea maandamano ya wahudumu wa matatu na baadhi ya washikadau wa sekta ya uchukuzi katika maeneo tofauti nchini leo Mei 18, huku baadhi ya barabara zikishuhudia usumbufu mkubwa wa usafiri.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha runinga nchini, Waziri wa Hazina ya Kitaifa, John Mbadi, alikosoa maandamano hayo akisema hayatoi suluhu ya kudumu kwa changamoto iliyopo.
Kwa mujibu wa Mbadi, hali ya sasa ya bei ya mafuta imeathiriwa kwa kiwango kikubwa na mvutano wa kimataifa unaohusisha Marekani, Israel na Iran, ambao umechangia kuyumba kwa soko la mafuta duniani.
“Maandamano haya hayawezi kushusha bei ya mafuta. Serikali inaendelea kutafuta njia mbadala za kudhibiti gharama hizi,” alisema Mbadi.
Aidha, Waziri huyo aliwashutumu baadhi ya wanasiasa kwa kile alichodai ni kutumia suala la bei ya mafuta kujijenga kisiasa badala ya kutafuta suluhu ya pamoja.
Hata hivyo, serikali bado haijaweka wazi iwapo ongezeko jipya la bei limetokana na shehena mpya ya mafuta iliyowasili nchini mwezi Aprili au changamoto za kimkakati katika uhifadhi wa mafuta nchini Kenya.
Mbadi alisema serikali imekuwa ikitekeleza hatua mbalimbali za kupunguza makali ya ongezeko hilo, zikiwemo:
Kuagiza mafuta kutoka mataifa tofauti
Kutumia mfumo wa serikali kwa serikali (G-to-G)
Kupunguza baadhi ya ushuru wa mafuta
Kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
Wakati huo huo, serikali imetangaza kikao cha dharura kitakachowakutanisha Waziri wa Kawi, Opiyo Wandayi, Waziri wa Barabara na Uchukuzi, Davis Chirchir, viongozi wa vyama vya uchukuzi pamoja na wadau wengine muhimu katika sekta hiyo.
Lengo la kikao hicho ni kutafuta mwafaka wa haraka wa kusitisha maandamano yanayoendelea huku serikali ikitafuta mbinu za muda mrefu za kudhibiti bei ya mafuta na kupunguza mzigo kwa wananchi.
Taarifa ya Elizabeth Mwende
News
Kaunti ya Kilifi yatenga shilingi milioni 10 kusimamia wajane kwa SHA
Serikali ya kaunti ya Kilifi imedai kwamba imetenga shilingi milioni 10 kusimamia huduma za afya kwa wajane
Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro aliwataka wajane na wanawake ambao bado hawajajisajili katika SHA, kutumia fursa hiyo ili iwe rahisi kwao kupata huduma za matibabu hospitalini.
Mung’aro aliwataka Wanawake wa kaunti ya Kilifi kuanza mchakato wa kuwasajali wajane katika SHA, akisema serikali ya kaunti iko na mipango ya kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma za matibabu bila changamoto.
Kiongozi hiyo pia alisema mikakati mwafaka imeidhinishwa kuhakikisha changamoto za urithi wa mashamba kwa akina wajane inashughulikiwa kupitia mawakili wa serikali ya kaunti.
“Naibu wangu ni mama, tuko na maafisa watano ni mama, kwa hivyo ni wajapange washirikiane na mawakili wa kaunti ili kupata haki ya urithi na tumetenga shilingi milioni 10 kusaidia wajane kujiandikisha na SHA ili wapate huduma za matibabu bila changamoto”,alisema Mung’aro.
News
Serikali imepiga marufuku uagizaji wa dawa za Antibiotiki kwa umma
Serikali imepiga marufuku uagizaji wa dawa za Antibiotiki na kusafirishwa na wahudumu wa bodaboda katika makaazi ya umma, ikisema mwenendo huo hautakubalika.
Waziri wa Afya nchini Adan Duele amesema serikali kupitia Wizara ya Afya nchini na Bodi ya dawa na sumu nchini zimeweka mikakati mwafaka ya kulinda afya ya wananchi.
Duale alisema wakenya hawafai kuilaumu bodi ya dawa na sumu nchini kutokana na sheria ngumu ilizotoa bali kuridhia hatua hiyo ili kuzuia madhara.
Akizungumza wakati wa warsha ya mikakati ya kuboresha afya ya umma, Waziri Duale alisema hatua hiyo inaanza kutekelezwa mara moja, huku akisisitiza kwamba serikali haitalegeza kambi katika kulinda afya ya umma.
“Kuanzia sasa hakuna tena kuagiza dawa za antibiotiki na kusafirishwa na wahudumu wa bodaboda kwani hatua hiyo ni hatari, wewe uko nyumbani kisha unaagiza dawa sini hiyo ni hatari, na hakuna kulaumu bodi ya dawa na sumu nchini kwa sababu tumeweka sheria hiyo”, alisema Duale.

Warsha ya watafiti wa kisayansi iliyiofanyika jijini Nairobi
Waziri huyo wa Afya nchini alishikilia kwamba hatua waliochukua mwafaka kwani italinda afya ya wananchi, akiwaonya wale wanaoendeleza bishara hiyo haramu. kusababisha madhara.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

