National News
KUPPET Yataka Walimu Kupewa Usalama
Naibu katibu wa Chama cha Walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri nchini KUPPET kaunti ya Kilifi Opollo Zacharia Kopolo ametoa wito kwa serikali kuu kuhakikisha walimu ambao wanafunza katika maeneo ambayo hayana usalama wa kutosha kuimarishiwa usalama.
Kopolo amesema hatua hiyo itachangia kuzikabili changamoto mbalimbali ambazo walimu hao wamekuwa wakipitia na kuchangia matokeo duni ya elimu.
Kopolo amesema ni jukumu la serikali kuu kuhakikisha walimu wanafanya kazi katika mazingira bora kwani imekuwa vigumu kwao kuwafunza wanafunzi ipasavyo kama wanafunzi wengine nchini.
Vilevile, Kopolo amesema kuna baadhi ya walimu ambao wamekuwa wakikataa kufunza katika maeneo hayo ambayo yanakabiliwa na utovu wa usalama wakihofia usalama wao hali ambayo inachangia kwa wanafunzi kuandikisha matokeo duni.
National News
Umoja wa mataifa wapunguza bajeti yake kwa bola milioni 577
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amependekeza kupunguzwa kwa bajeti ya umoja huo ya mwaka ujao kwa dola milioni 577, hatua ambayo itapunguza asilimia 18 ya kazi.
Akizungumza mbele ya kamati ya bajeti ya Baraza kuu la umoja wa mataifa, Guterres alisema umoja huo bado haujapokea mchango wa karibu dola milioni 900 kutoka kwa wanachama mwaka huu wa 2025.
Umoja wa mataifa unapendekeza bajeti ya dola bilioni 3 kwa mwaka 2026, ikiwa na upungufu wa asilimia 15 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka huu.
Umoja wa Mataifa unakabiliwa na mgogoro wa kifedha uliosababishwa pakubwa na hatua ya Marekani kutolipa ada yake, kutokana na sera mpya za Rais Donald Trump.
Hatua hii ya umoja wa mataifa huenda ukachangia changamoto kubwa kwa mataifa wanachama hasa yanayotegemea pakubwa juhudi za umoja huo katika masuala mbalimbali ikiwemo usalama.
Editor's Picks
Bangi Yanaswa Daraja la Sabaki – Malindi, Kaunti ya Kilifi
Maafisa wa Usalama wamenasa shehena ya Bangi katika daraja la Sabaki, Mjini Malindi Kaunti ya Kilifi, iliyokuwa imefichwa kwenye makasha ndani ya basi lililokuwa likisafiri kitoka Lamu kwenda Mombasa.
Basi hilo lilisimamishwa na Maafisa wa usalama katika kizuizi Cha Polisi kilichoko daraja hilo kwa shughuli ya kawaida ya ukaguzi wa magari na mizigo, ambapo magunia mawili ya bangi hiyo yalipatikana yamefichwa katika sehemu ya Mizigo ndani ya basi hilo.
Dereva na Kondakta wa basi hilo, mali ya kampuni ya mabasi ya Tawakal, walikamatwa, ingawa abiria anayeaminika ndiye mwenye kusafirisha bangi hiyo alitotoka mtego huo na bado anatafutwa na Maafisa Polisi.
Waliokamatwa sasa wanazuiliwa katika kituo cha Polisi cha Mjini Malindi huku uchunguzi zaidi unapoendelea.
Maafisa hao wanasema, walipata vidokezo kuhusiana na bangi hiyo ambayo bado haijajulikana thamani yake.
Katika siku za hivi karibuni, Daraja hilo la Sabaki limekuwa chini ya oparesheni kali ya maafisa wa usalama kutokana kuongezeka Kwa idadi ya vyombo vya usafiri, hasa Malori ambayo yaaminika kutumika kwa zaidi kwa biashara haramu kutoka Kaunti za Tana River na Lamu kuingia Kaunti za Kilifi na Mombasa.
Dereva huyo na Kondakta wake watafikishwa mahakamani hivi karibuni huku maafisa wa Polisi wakitia wito kwa wanachi kutoa habari zitakazosaidia kumtia nguvuni mshukiwa mkuu.

