News
NGEC, yasisitiza udhibiti wa dhulma za kijinsia
Tume ya jinsia na usawa NGEC inasisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wanaume ili kudhibiti visa vya dhuluma za kijinsia nchini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mkakati wa miaka mitano ya tume hiyo, Waziri wa jinsia nchini Hanna Cheptumo alisikitishwa na ongezeko la visa vya ukatili wa kijinsia na kusisitiza umuhimu wa kuwahusisha vijana na watu walio na uatilifu ili kudhibiti dhuluma mbalimbali na kuleta usawa katika jamii.
Vile vile, Cheptumo alishinikiza uwekezaji kwenye miradi ya kuwawezesha kiuchumi wanawake, watu walio na uatilifu na vijana.
Cheptumo alisema iwapo watu walio na uatilifu, vijana na wanawake watawezeshwa ipasavyo wataweza kujikimu kimaisha na hata familia zao bila kutegemea misaada na kusisitiza kwamba hakuna mtu yeyote ambaye anapaswa kubaguliwa kwa namna yoyote ile.
“Kifungu cha 27 cha Katiba ya nchi ya mwaka wa 2010, inampa kila mtu haki ya usawa na uhuru dhidi ya ubaguzi wa aina yoyote’’ Alisema Cheptumo.
Kwa upande wake msemaji wa serikali Isaac Mwaura alitoa wito kwa watu walio na uatilifu kuweka juhudi zaidi katika kujiendeleza kimaisha badala ya kusubiri msaada kutoka kwa mashirika mbalimbali na serikali huku akiwataka kujikubali na kupuuza yale ambayo yanasemwa kuhusu hali zao kwani wana uwezo kama wanadamu wengi.
“Kama watu walio na uatilifu mtapitia unyanyapaa mwingi kutoka kwa watu hasa mnapopata nafasi za uongozi kwa sababu kuna watu wanaona hamstahili’’ alisema Mwaura.
Taarifa ya Janet Mumbi
News
Polisi wanachunguza tukio la wizi dhidi ya raia wa kigeni
Maafisa wa Polisi kaunti ya Mombasa wanachunguza tukio la wizi dhidi ya mtalii wa kigeni lililotokea katika eneo la Nyali
Kulingana na ripoti ya maafisa wa polisi, mtalii huyo mwenye umri wa miaka 51 ambaye ni raia wa Marekani, anadai kulaghaiwa na kisha kushambuliwa na kundi la wanaume aliyokutana nao muda mfupi kabla ya tukio.
Ripoti hiyo imeeleza kwamba mnamo mwezi Aprili 9 mwaka huu, raia huyo wa kigeni akiwa katika mkahawa mmoja eneo la Nyali jijini Mombasa, alikutana na mwanaume aliyejitambulisha kama Alex, ambaye alimshawishi kuelekea katika nyumba ya Airbnb iliyoko karibu na mkahawa huo.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kwamba alipofika katika chumba hicho, alikumbana na wanaume wengine watano waliokuwa wakimsubiri ambapo mlango ulifungwa na kisha akashambuliwa na kulazimishwa kutoa pesa na vitu vya thamani.
Wahalifu hao walitoroka na mali mbalimbali ikiwemo simu ya rununu, kompyuta mpakato (laptop), fedha taslimu pamoja na fedha za kigeni na pia walifanikiwa kutoa pesa kutoka kwenye kadi zake za benki kwa njia ya udanganyifu.
Maafisa wa polisi kutoka Bamburi kwa kushirikiana na maafisa wa upelelezi wa DCI Nyali walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, ingawa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa wala mali iliyopatikana.
Kesi hiyo imewekwa chini ya uchunguzi zaidi huku juhudi zikiendelea kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
News
Polisi eneo la Likoni-Mombasa inachunguza kifo cha mwanamke
Idara ya usalama eneo la Likoni kaunti ya Mombasa imesema inachunguza kifo cha mwanamke mmoja aliyefariki katika mtaa wa senti kumi.
Mkuu wa polisi wa Likoni Joseph Mutungi alisema mwanamke huyo anadaiwa kupoteza maisha wakati wakiwa nyumbani kwa mwanamme anayesemekana kuwa mchumba wake.
Taarifa za awali ziliarifu kuwa marehemu alikuwa mgonjwa na anadaiwa alifika hospitalini kusaka matibabu japo hakupata huduma na kurejea nyumbani bila kutibiwa.
Inasemekana baadaye mchumba wake alioondoka kwenda kazini na kumwacha chini ya uangalizi wa mwanamke mwengine katika ploti hiyo.
Hali yake inadaiwa kuzorota na hatimaye kuaga dunia.
Maafisa wa usalama walisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho.
Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Coast general kwa uchunguzi zaidi.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

