News
Usalama umeimarishwa kabla ya ziara ya Rais Ruto, Kilifi
Serikali imesema usalama umeimarishwa katika kaunti ya Kilifi kabla ya ziara ya rais William Ruto juma lijalo katika halfa ya uzinduzi wa ujenzi wa uwanja wa kitaifa katika eneo la Tezo na miradi mingine zaidi ya 20 kaunti ya Kilifi.
Kamishna wa kaunti ya Kilifi David Wanyonyi na Katibu katika Idara ya ulinzi nchini Dkt Patrick Mariru, wamesema maafisa wa usalama wanashika doria katika kila sehemu ya kaunti ya Kilifi.
Akizungumza na Wanahabari baada ya ukaguzi wa matayarisho ya ujenzi wa uwanja wa Ronald Ngala katika eneo la Tezo kaunti ya Kilifi, Katibu katika Wizara ya ulinzi nchini Dkt Patrick Mariru amesema mipango na mikakati imeandaliwa.
Kamishna wa kaunti ya Kilifi David Wanyonyi amesema vitengo mbalimbali vya kiusalama vinashirikiana kuhakikisha visa vya utovu wa usalama vinakomeshwa ili kufanikisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Katika katika Wizara ya ulinzi Dkt Patrick Mariru afanya ukaguzi wa ujenzi wa uwanja wa Ronald Ngala, eneo la Tezo kaunti ya Kilifi
Wanyonyi alisisitiza kwamba vikundi vya kihalifu vitakabiliwa kwani maafisa hao wanashika doria pia katika miji mkuu ikiwemo Kilifi, Malindi, Watamu na Mtwapa huku onya kukomeshwa visa vya dhulma za kijinsia.
Kwa upande wake Kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa ambaye pia ni Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya amesema ziara ya rais Ruto ni mafanikio makubwa kwa wakaazi wa Kilifi kwani zaidi ya miradi 20 itazinduliwa.
News
Wadau wa sekta ya uchukuzi wasitisha mgomo wao
Maafisa wa sekta ya uchukuzi wameahirisha mgomo wao baada ya mazungumzo yaliyoongozwa na Rais William Ruto katika ikulu ya Mombasa.
Maafisa hao wakiongozwa na rais wa Muungano wa wamiliki wa matatu Albert Karagacha wamesema kuwa mengi ya masuala waliokuwa nayo ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta nchini yameangaziwa kwa kina na rais Ruto.
Karagacha amewataka wahudumu wa sekta ya uchukuzi wa umma pamoja na wamiliki wa magari ya uchukuzi wa mizigo kuhakikisha wanarudisha magari yao barabarani, akisema masuala waliowasilisha kwa rais yameangaziwa
Akizungumza mda mfupi baada ya kufanya kikao na rais William Ruto mjini Mombasa, Karagacha amesema serikali imekuwa kiangazia kwa kina masuala mbali mbali yanayohusu sekta ya uchukuzi nchini.
Aidha amesema iwapo bado serikali itakuwa inajikokota katika kufanikisha masuala waliojadiliana basi wataitisha mazungumzo zaidi na Wizara husika ili kuafikiwa kwa ajenda zao huku akisema japo suala la mzozo wa mafuta sio jambo la Kenya pekee lakini taifa inawajibu wa kusaidia wananchi wake.
Wakati huo huo Karagacha amewataka wakenya kutoingiza siasa katika suala la kupanda kwa bei ya mafuta nchini.
Taarifa ya Joseph Jira
News
Mshukiwa wa ulanguzi na usafirishaji wa watoto anyimwa dhamana
Mahakama ya Shanzu imemnyima dhamana mshukiwa wa ulanguzi wa watoto zaidi ya 20.
Mahakama imeagiza mshukiwa huyo kuzuiliwa rumande ili kuwawezesha maafisa wa polisi kukamilisha uchunguzi wao.
Mahakama imeelezwa kwamba mshukiwa huyo Almasi Rama Amos mwenye umri wa miaka 27 alikamatwa na maafisa wa upelelezi kutoka kitengo cha kupambana na ulanguzi wa binadamu na ulinzi wa watoto (AHTCPU) pamoja na maafisa wa idara ya upelelezi wa Jinai kutoka kaunti ya Mombasa.
Kukamatwa kwake kufuatia wiki kadhaa za uchunguzi kuhusu ripoti za unyanyasaji wa watoto zinazowalenga wasichana wadogo walio katika mazingira magumu.
Rama, anayetuhumiwa kwa kujihusisha na kundi linalodaiwa kuwa la ulanguzi wa watoto na dhulma za kingono na kufikishwa katika Mahakama ya Shanzu kufuatia operesheni ya kiusalama iliyoidhinishwa na maafisa hao.
Rama alipatikana katika mtaa wa Nguu Tatu eneo la Concordia katika kaunti ndogo ya Kisauni akiwa na watoto watatu wa kike.
Mahakama imeelezwa kuwa mshukiwa anadaiwa kuendesha “vituo vya uokoaji” katika kaunti za Mombasa na Kilifi kwa kujifanya kuwalea na kuwapa ushauri.
Kulingana na uchunguzi vituo hivyo vilikuwa vikitumika kama msingi wa dhulma za kingono na unyanyasaji wa watoto.
Alipokamatwa, mshukiwa aliwaongoza maafisa hadi kituo chengeni eneo la Ribe katika eneo bunge la Rabai, ambapo maafisa wa upelelezi waliwaokoa watoto 19 wa jinsia ya kike na kufikisha jumla ya waathiriwa waliookolewa kufikia ishirini na wawili (22).
Mbele ya Mahakama ya Shanzu tarehe 21 Mei, 2026, mshukiwa amekabiliwa na mfululizo wa mashtaka, ikiwemo unajisi, biashara ya watoto kwa madhumuni ya kuwadhulumu kingono pamoja na unyanyasaji wa watoto ambapo amekana mashtaka hayo.
Kesi hiyo imepangwa kutajwa Juni 8, 2026.
Taarifa ya Teclar Yeri

