News
Wakenya waonywa dhidi ya kuchipuka kwa magonjwa msimu wa mvua
Wizara ya Afya nchini imewarai wakenya kuchukua tahadhari ya mapema msimu huu wa mvua na kutibu maji wanayotumia kila siku ili kuepuka kukumbwa na magonjwa mbalimbali.
Katibu katika Idara hiyo Mary Muthoni, alisema baadhi ya maeneo yanashuhudia mvua nyingi na huenda ikaathiri wananchi iwapo hawatakuwa maniki dhidi ya kujikinga na magonjwa.
Alisema mara nyingi magonjwa wengine huchangiwa na mazingira machafu, na maji yaliochanganyika na maji taka, akisisitiza haja ya wananchi kuwa makini na kuhakikisha wanachamsha maji ya kunywa kwa usalama wao.
Katibu huyo alisema watu wengi wamekuwa na hulka ya kutumia maji ya visima na mabwawa na mara nyingi huwa na chembechembe ya viini, akisisitiza haja ya wananchi kuchukua tahadhari ya kutibu maji ama kuchemsha maji ya kunywa kabla ya kuyatumia ili kuepuka maambukizi ya maradhi mbalimbali.
Akizungumza katika kaunti ya Nyeri, Muthoni aliwarai wananchi kutopuuza tahadhari hiyo na kuhakikisha wanalinda afya zao.
“Kuna athari ya kuchupuka kwa magonjwa mbalimbali kama yale ya kuendesha kutokana na uchafuzi wa mazingira na utumizi wa maji ambayo hajatibiwa ama kuchemshwa, kwa hivyo langu ni kuwahimiza wananchi wachukue tahadhari ya mapema hasa msimu huu wa mvua ili kuepuka magonjwa”, alisema Muthoni.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
News
Jubilee yaunga mkono maandamano ya kupinga bei ya mafuta
Kufuatia sakata ya uagizaji wa mafuta ghushi nchini, sasa Muungano wa upinzani umetishia kufanya maandamano kuanzia wiki ijayo.
Mwenyekiti wa kitaifa wa Chama cha Jubilee Vincent Kemosi, alisema maandamano hayo yanalenga kushinikiza kupunguzwa kwa bei ya mafuta nchini, akimshtumu Rais William Ruto kwa kuchangia mahangaiko wakenya.
Katika kikao na Wanahabari mjini Kilifi kaunti ya Kilifi baada ya kufanya kifanya kikao na viongozi wa chama hicho kanda ya Pwani, Kemosi aliikosoa serikali, akisema wakenya wamechoka kudanganywa na serikali iliyofeli kutekeleza ahadi zake.
“Serikali imeonyesha kushindwa kutatua suala la mafuta na imeonyesha wazi kwamba imefeli, huezi badilisha ushuru wa mafuta baada ya wananchi kulalamika mbona hakufanya hivyo tangu mwanzo, wakenya wamechoka”, alisema Kemosi.
Kemosi, amepinga mpango wa kugawa maeneo kisiasa yaani Zoning, akisema Viongozi wa Chama cha Jubilee watazingatia haki na usawa pamoja na kuandaa uchaguzi wa mashinani wa viongozi wa chama hicho, kauli iliyoungwa mkono na Mwenyekiti wa chama hicho kaunti ya Kilifi Anthony Kingi.
“Katika ya Kenya haijasema mambo ya Zoning, kila mtu ana haki ya kupigania wadhfa anataka, na sisi kama Chama cha Jubilee hatuingi mkono mambo ya zoning, tutahakikisha uchaguzi unafanyika mashinani kwa haki na uwazi”aliongeza Kemosi.

Viongozi wa Chama cha Jubilee wakiongozwa na Mwenyekiti wa kitaifa wa Chama hicho wafanya mkutano wa kuimarisha chama mashinani, Kilifi
Viongozi hao pia waliwarai wananchi kutathmini viongozi wao na kujiunga na vyama vinavyozingatia haki na usawa, wakisisitiza kuunga mkono upinzani.
Katika swala la raslimali, viongozi hao wameshtumu kutengwa kwa raslimali za Pwani hasa zao la mzani na mkorosho, wakisema wakati umefika kwa mpwani kutambulika na raslimali zake kuthaminiwa.
“Zao la Mnazi na Mkorosho ambayo ndio raslimali ya mpwani imetengwa tangu taifa ipate uhuru ndio sisi tunasema ni lazima raslimali ya mpwani pia nayo itambulike kikamilifu”, alisema Garama.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi.
News
Meli yenye bendera ya Kenya yazuiliwa Tanzania
Mamlaka ya usafiri wa majini nchini (KMA), imethibitisha kupokea taarifa kuhusu kuzuiliwa kwa meli yenye bendera ya Kenya katika nchi ya Tanzania.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, KMA imesema meli hiyo inayojulikana kama MV SEA MFALME kwa sasa inashikiliwa nchini humo.
Maafisa wa Mamlaka hiyo, wale wa ujasusi, na wanajeshi wa majini wameanzisha uchunguzi kubaini sababu za tukio hilo, na kama meli hiyo ilikuwa imebega shehena gani ndiposa ikazuiliwa.
Mamlaka hiyo imeeleza kuwa inashirikiana kwa karibu na mashirika ya kiserikali pamoja na wadau katika nchi zote mbili ili kubaini kilichosababisha kuzuiliwa kwa meli hiyo na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa.
Mamlaka hiyo ilielezwa kwamba tayari imeijulisha Wizara ya masuala ya kigeni nchini inayoongozwa na Waziri Musalia Mudavadi ili kusaidia katika masuala ya kidiplomasia kwani hatua hiyo huenda ikachangia sintofahamu za kimataifa.
KMA imewahakikishia wadau wa sekta hiyo na wamiliki wa meli hiyo kuwa suala hilo linashughulikiwa kwa kufuata taratibu za kisheria na ushirikiano wa kimataifa, na kwamba taarifa zaidi zitatolewa kadri uchunguzi unavyoendelea.
“Tunashirikiana na wadau mbalimbali kwa kuzingatia sheria za kimataifa na ushirikiano wa kidiplomasia kuhusu suala hilo na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa”, alieleza afisa mmoja wa Mamlaka hiyo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu

